Jeshi la Wananchi la Uganda (UPDF) limewashambulia waasi wa kikundi cha Allied Democratic Forces (ADF) cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

ADF wanahusishwa na shambulizi la Desemba 7, mwaka huu lililofanyika kwenye kambi ya askari hao ya Simulike, Mashariki mwa DRC na kusababisha vifo vya askari 15 na wengine 44 kujeruhiwa.

Gazeti la Daily Monitor la Uganda limemkariri Msemaji wa UPDF, Brigedia Richard Karemire, akisema ndege za kivita za nchi hiyo ziliishambulia ngome ya waasi wa ADF mchana wa Ijumaa iliyopita.

“Tumeishambulia ngome ya waasi wa ADF kule DRC mchana (ijumaa). Wana intelijensia wa Uganda na DRC wamethibitisha kuwa magaidi wa ADF ambao hivi karibu waliwashambulia walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa walio chini ya MONUSCO, walikuwa wanapanga kufanya vitendo vya hujuma dhidi ya Uganda,” amesema.

Ameongoza, “ili kuwawahi mapema, mchana wa leo (Ijumaa) UPDF ilishambulia kambi zao kule mashariki mwa DRC.”

“Wanachokisubiri magaidi wa ADF ni muda ufike, watalengwa popote watakapojificha,” amesema.

Brigedia Karemire amesema mashambulizi ya UPDF dhidi ya ADF yalifanyika kwa ustadi mkubwa wa kutumia silaha na ndege za kivita zinazompiga adui kutoka masafa marefu, hivyo askari wake hawakuingia nchini DRC.

Shambulizi la ADF limefanyika takribani siku 16 baada ya shambulizi la Desemba 7 dhidi ya askari wa Tanzania. Mbali na Watanzania, askari wengine watano wa DRC waliuawa katika shambulizi hilo.

Alhamisi iliyopita, magari kadhaa yaliyowabeba askari wa Uganda ambao idadi yao haikufahamika, wakiwa na vifaa vya kijeshi yalionekana kwenye mji wa Fort Portal yakielekea Bundibugyo.

Msemaji Msaidizi wa UPDF, Meja Peter Mugisa, amewaambia waandishi wa habari hatua ya kulipeleka jeshi kuwakabili ADF kulitokana na taarifa kuwa waasi hao walipanga kuingia Uganda kupitia wilaya ya Bundibugyo.

Kwa mujibu wa Meja Mugisa, askari wa Uganda walipangwa kuyadhibiti maeneo yote yanayosadikiwa kuwa njia za waasisi wa ADF.

Kwenye miaka 1990, waasi wa ADF waliingia kwenye maeneo ya Wilaya za Kasese, Bundibugyo na Kabarole katika Mkoa wa Rwenzori na kufanya hujuma zao kwa zaidi ya muongo mmoja.

Waasisi hao walisadikiwa kuwaua zaidi ya watu 3,000 na kusababisha wengine kiasi cha 100,000 kukosa makazi.

Hata hivyo, Brigedia Karemire hakufafanua kuhusu hali za waasi baada ya mashambulizi hayo kwa madai kwamba UPDF bado inafanya tathmini.

Msemaji wa Wilaya ya Bundibugyo, Ronald Mutegeki, amesema Shule ya Msingi Busunga iliyopo takribani kilomita saba kutoka mpaka mwa Uganda na DRC itatumika kuwahifadhi wakimbizi kutoka mashariki mwa DRC.