Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ifikapo Agosti 12,Serikali imesema itaendelea kuzingatia matumizi ya fursa za kidijitali kwa vijana ili kuwapa fursa ya maendeleo endelevu kwa kuwapatia ujuzi wa kidijitali ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye nchini.

Hayo yameelezwa leo Agosti 9,2024 Jijini hapa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Patrobas Katambi kwenye mkutano wake na Waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika kitaifa mwaka huu 12 Agosti, Mkoani Dodoma.

Aidha kauli mbiu ya mwaka huu ni “Vijana na matumizi ya fursa za kidijitali kwa maendeleo Endelevu”kauli inayozisisitiza jumuiya za kimataifa kuwekeza kwa vijana kwa kuwaunganisha na fursa za kidijitali kwa sababu ulimwengu wa sasa umetawaliwa na matumizi ya teknolojia ya kidijitali kama vile matumizi ya simu, pamoja na uvumbuzi unaotokana na akili mnemba (Artificial inteligency).

Amesema kuwa siku ya vijana inawakilisha ndoto, matumaini, na nguvu za kizazi kipya ikiwa ni pamoja na kutoa fursa ya kipekee kwa vijana kuonyesha uwezo wao, kuungana, na kujitolea kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla huku akisisitiza kuwa Vijana ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote.

“Katika nyakati hizi za mabadiliko ya haraka na changamoto, vijana wanachangia kwa kiwango kikubwa katika sekta mbalimbali kama vile teknolojia, elimu, afya, na biashara,tunawapongeza kwa juhudi zao na kujitolea kwa dhati,” amesema

Katambi ameeleza kuwa Serikali Katika kutekeleza majukumu yake inaendelea kuweka mikakati maalum ya kuunga mkono na kukuza vijana pamoja na kuimarisha elimu na mafunzo kwa vijana ambapo tayari imeshaanza kupanua fursa za ajira, na kutekeleza miradi ya kuboresha mazingira ya biashara kwa vijana.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa vijana wanapata rasilimali na usaidizi wanaohitaji ili kufikia malengo yao na kuwa sehemu ya mchakato wa maendeleo,tunapotimiza siku hii, ni muhimu pia kukumbuka kwamba changamoto bado zipo,tunahitaji kuimarisha ushirikiano kati yetu, sekta binafsi na jamii ili kuondoa vikwazo na kuongeza fursa kwa vijana, “amesema

Amefafanua kuwa Siku ya Vijana ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya vijana itaanza kwa kutekeleza shughuli mbalimbali ambapo Agosti 10 na 11, 2024 kutakuwa na kongamano la vijana litakalofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

“Kongamano hilo litahusisha vijana 3,000 kutoka katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar ambapo Kupitia kongamano hilo, vijana watajadili masuala mbalimbali ikiwemo kutoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo (Tanzania tuitakayo 2050), vijana na matumizi ya fursa za kidijitali, vijana na uchumi, afya ya akili, na saikolojia ya vijana, “amefafanua Katambi

Naibu waziri huyo pia amesema Agosti 12, 2024, itakuwa ni siku ya kilele cha kuadhimisha Siku ya Vijana Kimataifa, ambapo vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana watashiriki huku Mgeni rasmi wa maadimisho ya mwaka huu anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (

“Itambulike kwamba, vijana ndio kundi kubwa, kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15-35 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 21,312,411 sawa na (34.5%) ambapo kwa Tanzania bara ni 20,612,566 sawa na (34.4%),

Kwa kutambua kuwa vijana ndio nguvu ya kufanya kazi, wabunifu na chachu ya mabadiliko katika jamii yoyote ile,Pia Vijana ndiyo warithi wa historia katika Mataifa yao na kwa mantiki hii hatuna budi kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika maendeleo ya nchi yetu.

Please follow and like us:
Pin Share