Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) imetoa wito kwa wakulima nchini kuendelea kutumia mbegu za asili ili zisiweze kupotea.

Wito huo umetolewa na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhifadhi wa Bioanuai kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), Dkt. Neduvoto Mollel wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane).

“Mbegu za asili zina ladha nzuri kulinganisha na mbegu ambazo zimeshabadilishwa. Kwahiyo tunawasisitiza na kuwashauri wananchi waendelee kuziendeleza mbegu hizi.

“Athari ambayo Taifa linaweza kukumbana nalo iwapo mbegu za asili zitapotea ni kuwa tegemezi kwa mbegu zinazoingizwa kutoka kwa watu wengine hivyo, kama nchi ni lazima iwe na hifadhi ya kutunza mbegu mama likitokea lolote tuwe na mahali pa kuanzia,” amesema.

Amefafanua kuwa, TPHPA imeanzisha benki za jamii katika maeneo ya Karatu na Kusini mwa Tanzania ambapo wanawafundisha wakulima namna ya kutunza mbegu.

“Kwahiyo tuko hapa Nanenane tunatoa elimu na tunawahamasisha wakulima wahakikishe mbegu za asili hazipotei, yeyote mwenye mbegu ya asili au anayependa kuendeleza mbegu ya asili aje achukue sampuli na kutumia,” amesema Dk. Mollel.

Amesema wanahifadhi mbegu za asili za mazao ya Mahindi, Mpunga, Maharage, Mchicha, Maboga, Alizeti, Dengu na nyingine.

“Wakulima wengi wamepita katika banda letu wamechukua sampuli za mbegu za asili na wengi wanatamani za mahindi na maboga, wanatamani kupata ladha ya zamani, tunawapa sampuli wakazioteshe lakini wakiwa wanajua kwamba ni mbegu za asili za zamani ili zisipotee, bado kuna wakulima wanazo wanazihifadhi na zinatunzika bila madhara yoyote,” amesema.

Amesema pia wana kitengo cha hifadhi ya sampuli kavu za mimea na taarifa zake ambazo zinahifadhiwa kwa ajili ya rejea ya baadaye na uhifadhi wa misitu ili kujua ambazo ziko kwenye hatari ya kupotea kutokana na uchache wake au mabadiliko ya tabianchi.

Please follow and like us:
Pin Share