Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetoa tuzo kwa waandishi wa habari, wachora katuni na wapigapicha bora. Hili ni tukio jema. Linapaswa kuungwa mkono. Rais Jakaya Kikwete ameliona hilo, ameahidi kuwa Serikali itashiriki.
Nawapongeza kwa dhati wote walioamua kukusanya kazi zao na kuziwasilisha MCT kwa ajili ya tuzo hizo. Kwa namna ya pekee, nawahimiza waendelee kuitumikia jamii yetu kwa moyo na ujasiri wa hali ya juu.
Hata hivyo, nina maoni kidogo. Kwa kuwa suala la tuzo ni motisha na changamoto kwa wanahabari, nadhani kuwapo kwa mawazo mbadala kunaweza kusaidia kuboresha jambo hili mbele ya safari, hasa ikizingatiwa kuwa tupo wengi tunaoliunga mkono jambo hilo jema lililoasisiwa na MCT.
Baraza limepata fedha nyingi kwa ajili ya kazi hiyo, ambayo bila shaka imelenga kuwahamasisha wanahabari ili waweze kutekeleza wajibu wao kwa juhudi na weledi wa hali ya juu.
Nampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa mapenzi yake kwa vyombo vya habari, ingawa siku hizi yamepungua. Wanahabari wengi sasa wanatamba na kuchanua kumetokana na ‘hisani na huruma’ yake.
Kwa sheria zetu za habari hapa nchini, kama Rais Kikwete angezisimamia vilivyo, leo tungebaki na TBC na magazeti mawili, matatu yenye uhusiano na Serikali.
Kwa hilo la uvumilivu walau tunapaswa kumshukuru, na kwa kweli anastahili pongezi. Kama alivyokomalia Katiba, matarajio yetu ni kuona sheria kandamizi zote zinafutwa ili tusiwe na uhuru wa habari wa hisani kama ilivyo sasa.
Rais Kikwete alipozungumza kwenye hafla hiyo tulimsikiliza kwa makini. Alitoa hotuba iliyosheheni changamoto nyingi. Baadhi ya mambo yaliyonivutia ni ya kuhamasisha wamiliki wa vyombo vya habari kuwalipa vizuri waandishi na watumishi wao, kudumisha umoja na mshikamano wa Tanzania; na kujenga moyo wa uzalendo kwa kuhakikisha wanahabari hawawi sehemu ya mawakala wanaotaka kuikwaza Tanzania kimaendeleo. Ilikuwa hotuba nzuri, na kwa kweli inastahili kuwa mwongozo yakinifu kwa wanahabari wote nchini.
Pili, tuzo ya vifaa na vyeti pekee haitoshi. Waliobuni kitu hiki wangekwenda mbali zaidi kwa kuona namna ya kuwasaidia wanahabari kujiendeleza kitaaluma. Kama kuna mpigapicha aliyeshinda, zawadi nzuri si kumpa kamera au fedha, bali ingekuwa kumpeleka ughaibuni akapata ujuzi na vionjo zaidi.
Kama kuna mwanahabari chipukizi aliyeibuka mshindi kwa kuandika habari ya uchunguzi, huyo angesaidiwa kupelekwa chuoni kujiongezea ujuzi ili baadaye afanye mambo makubwa zaidi kwa ajili ya jamii yetu. Hizi zawadi za kuishia kwenye kaya zao haziwezi kuwaongezea ujuzi.
Jambo jingine ninalopenda kulitolea maoni ni hili la namna ya kuwapata washiriki na washindi wa tuzo hizi. Utaratibu huu uliotumiwa na waandaaji unatumika sehemu nyingi duniani. Pamoja na ukweli huo, kuna umuhimu wa kubadili mfumo mzima. Si lazima tuige kila litokalo ughaibuni.
Kuwataka wanahabari wawasilishe kazi zao MCT ili hatimaye zipitiwe na kuwapata washindi, kunaweza kuwa si njia nzuri sana. Hiyo ingekuwa na maana zaidi kama mashindano yenyewe yangekuwa yanafanyika ughaibuni.
Lakini kama mashindano yanaratibiwa na kuhitimishwa hapa hapa nchini, kilichotakiwa si kwa wanahabari kuwasilisha kazi zao, bali kwa MCT na wadau wengine kuifanya kazi ya kuwapata washindi kulingana na uzito na ubora wa kazi zao.
Naamini kwa dhati kabisa kwamba aina hii ya kuwashindanisha wanahabari inaweza kuibua ‘kazi mbaya’ kutoka katika ‘kazi mbaya zaidi’ ikawa imeshinda.
Kwa maneno mengine ni kwamba njia hii inaweza kutoa kazi ambayo ni mbaya, lakini walau ni nafuu kati ya kazi nyingi mbaya zilizowasilishwa.
Naomba nieleweke hapa. Sibezi hata kidogo kazi zilizowasilishwa. Lakini kuna habari ya kujikuta mwaka mwingine majaji wakiamua kuteua kazi ambayo ‘kidogo ni afadhali’, huku wakiacha kazi nyingi ambazo hazikuwasilishwa kwenye mashindano.
Ni ukweli ulio wazi kuwa wanahabari wengi hawakuwasilisha kazi zao. Kwa kutowasilisha maana yake ni kwamba kazi zao hazikutambuliwa hata kama ni nzuri na zimekuwa na matokeo chanya katika jamii.
Sasa tufanye nini? Kwa kuwa MCT wana ukwasi wa kutosha, sioni ni kwanini kazi hii ya kuwasaka wanahabari wasiifanye wao kwa mwaka mzima ili hatimaye watupatie wanahabari nguli katika nyanja mbalimbali.
Wafuatilie vipindi vya redio. Wafuatilie vipindi katika televisheni. Wapitie magazeti na majarida ya kila siku. Wapembue habari wanazoamini kuwa kitaaluma zinajitosheleza kuingizwa kwenye mashindano.
Siku ya siku, watoke na majina ya wanahabari ambao kwa vigezo wanaamini kuwa wamefanya mambo ya kutukuka kwa jamii na taifa letu.
Aina hii ya kumpata mshindi inafanywa na Ubalozi wa Marekani kwenye tuzo ya ‘Mwanamke Mahiri’ na ile ya ‘Martin Luther King Jr.’ Ubalozi, kwa kutumia intelijensia yake, unafuatilia watu unaoona kuwa wamelifanyia taifa letu jambo jema la kutukuka. Mwisho wa siku wanamtaarifu mhusika na kumkabidhi tuzo.
Aina hii ya kumpata mshindi ina mvuto na kwa kweli ni heshima kubwa. Hata mimi naweza kujaa furaha nikibaini kuwa kuna watu wamenifuatilia na kubaini kuwa nina mchango wa kutukuka kwa jamii na taifa langu. Nikipewa tuzo kwa utaratibu huo, hakika hiyo furaha pekee itaniongezea siku za kuishi.
Lakini hii tuzo ya kukusanya magazeti na CD na kuvipeleka kwenye mashindano haiwezi kunipa raha. Kama tuzo yenyewe inayowaniwa ingelikuwa ni ya kimataifa ambayo huwezi kuwa na chombo kimoja cha kufuatilia kila mwanahabari dunia nzima, ningewaelewa.
La, kama waandaaji wanaona ni muhimu kuendelea na utaratibu huu wa mwanahabari kutia kwapani magazeti na CD na kuwapelekea, basi waongeze kipengele kingine kidogo – lakini muhimu.
Nacho ni kwamba wawe tayari wao wenyewe kufuatilia kazi zilizo katika redio, televisheni na magazeti kwa ajili ya kuona zile zilizokuwa na matokeo chanya katika jamii. Kazi hizo ziwe nje ya zile zilizowasilishwa na washindani. Hili wanaweza kulifanya kwa sababu wanazo fedha za kutosha.
Mwisho, niseme tu kwamba wanahabari waliofanya kazi za kutukuka kwa jamii na taifa lao, ambao hawakuwasilisha magazeti na CD kwa ajili ya kuzishindanisha ni wengi mno. Lakini kubwa ni kwamba mwandishi mwenyewe si lazima akajua moja kwa moja kama kazi yake imeweza kuwa na mrejesho chanya.
Kujua kama habari au picha imekuwa na matokeo chanya, hiyo ni kazi ya jamii. Na hapa Baraza na majaji ndiyo wanaopaswa kujiridhisha, hata kama ni kwa kuishirikisha jamii nzima ya wasomaji na wasikilizaji. Haya tunayaona hata kwenye soka.
Huwezi kumpata mchezaji bora wa mpira wa miguu kwa kutaka awasilishe mkanda wa video. Hivi kama ingekuwa hivyo, na ikatokea Lionel Messi akachelewa au akasita kuwasilisha mkanda wake kwa majaji, je, ni halali kumkosesha uchezaji bora wa dunia?
Je, kama Messi hawezi kuwasilisha mkanda, lakini kina Ngassa, Mafisango na wenzao wa kaliba hiyo wakawasilisha, ingenoga kweli kuona Ngassa akitangazwa kuwa mchezaji bora wa dunia kwa sababu tu Messi hakuwasilisha mkanda wake kwa ajili ya kushindanishwa naye?
Ndiyo maana nasema, pamoja na kuwaheshimu walioshinda tuzo hizi, bado nakosoa utaratibu unaotumika. Unaweza kuboreshwa zaidi. Naomba tena ieleweke kuwa naheshimu uamuzi wa majaji na ninawapa pongezi wote walioshinda.
Matarajio ya wengi ni kuona kuwa mengi yaliyozungumzwa na Mheshimiwa Rais Kikwete kwenye hafla hiyo, yanafanyiwa kazi.
Suala la ukata kwa wanahabari ni mjadala mzito. Hawalipwi, hata pale wanapolipwa, wanapunjwa. Kwenye malipo kuna sababu nyingi. Inawezekana hatulipwi vizuri kwa sababu baadhi yetu hatuna elimu ya kutuwezesha kudai malipo mazuri, au kwa sababu hatuna namna nyingine ya kuishi.
Kwa kuwa haya yamesemwa na Mheshimiwa Rais, matarajio yetu ni kuona vyumba vya habari kama vile New Habari Corporation waandishi na watumishi wake sasa wanalipwa kwa wakati. Waandishi wa habari tusipojitetea wenyewe, hakuna wa kututetea hasa kwenye ulimwengu huu wa ubepari.