Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
FUNDI Sanifu Mkuu Maabara kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Jacob Manguye amesema kuwa barabara nyingi zinafeli na kushindwa kuwa za kiwango kutokana na watu wengi kutokupima udongo kabla ya kuanza ujenzi.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwenye banda lao lililopo katika Maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kuwa ili Barabara itengenezwe Kwa ubora ni lazima ianze maabara kwa kupima sampuli za udongo, Kokoto au lami.
“Kwahiyo Tarura ina maabara ya kupima udongo ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kusimamia kazi, ubora wa barabara za kutoka vijijini hadi mijini ambazo zinateketezwa katika miradi mbalimbali nchini. Kazi ya maabara hiyo ni kuthibitisha ubora na kupitia maabara hii tunatarajia kuwa na kazi nzuri za kiwango zinazotakiwa ili kuondokana na kashfa za kazi kuwa chini ya kiwango,” amesema.
Amefafanua kuwa, kwasasa Barabara za Tarura zina ubora wa viwango vinavyotakiwa na kwamba wanajihidi kupanua Barabara hizo zipitike vijijini.
Kuhusu ushiriki wao katika maonesho ya Nanenane amesema kuwa Wakala huo umeshiriki kwa kuwa wana uhusiano na Wakulima na Wafugaji ambao hutumia Barabara kusafirisha mazao yao kupitia barabara ilizojenga.
“Kwahiyo tuko hapa kuonesha jinsi gani Tarura tunafanya kazi zetu na kutoa elimu kwa jamii ielewe kuhusu maabara yetu ,” amesema.