Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa

Raia wa Uswisi, Dk. George Hess, anatuhumiwa kujimilikisha na kuuza ardhi ya ufukwe wa Amboni uliopo Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, kinyume cha sheria. Dk. Hess, anayeishi nchini Kenya, kupitia tovuti yake ya ambonibeach.com, amejitangazia ‘Jamhuri’ katika eneo hilo, kuwa ndiye mmiliki pekee Tanzania mwenye ufukwe, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999.

Sheria ya Mipango Miji namba 7 ya mwaka 2008 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, inakataza mtu yeyote kumiliki ufukwe wa bahari bali fukwe zinapaswa kumilikiwa na umma. Lengo la kutungwa kwa sheria hiyo ni kuhakikisha fukwe hazihatarishi amani, ulinzi na usalama wa raia.

Pia sheria hizi zinalenga kupunguza uharibifu wa mazingira na kuwapa wananchi fursa ya kutumia fukwe za bahari kwa burudani, michezo na mambo mengine yenye tija nchini.

Mbali ya hilo, Dk. Hess pia kupitia tovuti hiyo, ametangaza kumiliki ardhi na kuiuza kinyume cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu cha 20 (1), kinachokataza wageni kumilikishwa  ardhi ikiwamo ya maeneo ya ufukweni.

“Kuepusha mkanganyiko, mtu asiye raia [wa Tanzania] hapaswi kupewa ardhi isipokuwa kama ni kwa malengo ya uwekezaji chini ya Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 1977,” kinasema kifungu hicho na kuongeza:

“Ardhi iliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji chini ya sehemu ndogo ya kwanza ya sheria hii inapaswa kutambuliwa, kutangazwa katika gazeti la Serikali na kukabidhiwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho kitatengeneza utaratibu wa haki ya mwekezaji kuitumia ardhi hiyo kuzalisha [si kuimiliki]”.

Tayari, Dk Hess ameuza viwanja tisa kwa watu mbalimbali kutoka nje ya nchi na wenyeji wapo waliojenga nyumba na wanaishi. Mmoja wa watu waliouziwa viwanja hivyo ni raia wa Zimbabwe mwenye asili ya Kireno, Martin Perela, na tayari amejenga nyumba na anaishi katika eneo hilo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Dk. Hess pamoja na sheria hiyo kukataza wazi, yeye anamiliki hati ya ardhi katika eneo hilo. Hati ya mwanzo ya miaka 99 aliyopewa wakati wa ukoloni ameikabidhi kwa kampuni ya Amboni Plantation Limited shamba la mkonge la Kigombe.

Ramani ya shamba hilo hadi sasa inaonesha kuwa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 12,000 lina hati moja na lilianzia katika Kijiji cha Kilale na kuishia Bahari ya Hindi. Baada ya kuuza shamba hilo kwa kuligawa vipande viwili, alikabidhi hati kwa Amboni Plantation Limited, hivyo ambonibeach.com ikabaki bila hati.

Mbali ya ufukwe huo, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa wageni wamekuwa wakimiliki fukwe nyingi katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan katika eneo la Kigamboni Dar es Salaam ambako wameuziwa na wenyeji.

Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa, alisema hana taarifa kuhusu umiliki na mgogoro wa shamba hilo.

Anasema hajawahi kuona au kusikia kuhusu mabadiliko ya matumizi ya shamba hilo, lakini ameahidi kufuatilia katika makabrasha ya Wilaya ya Muheza.

“Ninavyojua suala hili limevuka mipaka haliwezi kujadiliwa katika ngazi ya mkoa au wilaya hadi taifa, naomba uwasiliane na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, watakupa majibu,” amesema Galawa.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, amesema hataweza kushughulikia suala hilo kwa kuwa ana majukumu mengine.

“Hivi nani aliyekupa hizi habari? Bwana mie sina habari na hilo kwa sasa naangalia vipaumbele vya maji, elimu na kilimo kwa kuwa wananchi hawajaleta malalamiko yao kwangu.

“Mie silijui wakileta nitalishughulikia na kutoa majibu lakini wasiliana na DED (Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya) atakuwa na majibu,” amesema Mgalu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Ibrahm Mtovu, alipoulizwa alimtaka mwandishi kumpigia simu saa 9 alasiri, lakini alipopigiwa siku ya Jumanne muda huo, alipokea simu na kukata mawasiliano.

Alipopigiwa siku ya Ijumaa, Mtovu alipokea simu na baada ya mwandishi kujitambulisha alimtaka apige baada ya dakika tano. Baada ya dakika 10 Afisa Ardhi wa Wilaya Muheza, Selemani Kanunge, alipiga simu na kuiambia JAMHURI kuwa mgogoro huo upo na ni wa muda mrefu.

Amesema suala hilo limefanyiwa kazi na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kupitia vikao vya Kamati ya Ardhi. Waligundua suala hilo baada ya kusoma katika mtandao kuwa Dk. Hess anauza viwanja katika Ufukwe wa Amboni, wakamsimamisha na viongozi wa wizara wakafanya ukaguzi.

Amesema walimweleza utaratibu na akapeleka maombi katika Baraza la Ardhi la Wilaya na yakafanyiwa kazi kisheria.

Kanunge amesema walipeleka maombi yake kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kaskazini, Doroth Wanzala, naye akatoa kibali cha ardhi hiyo kupimwa.

Hata hivyo, amesema suala hilo bado lina mkanganyiko mkubwa kutokana na Dk. Hess kukataa kupima viwanja hivyo kwa ramani iliyoidhinishwa na wizara, badala yake anatumia yake.

Kanunge amesema Dk. Hess amekataa kupima viwanja hivyo kama inavyotaka ramani ya wizara, kwa kuwa haimruhusu kumikili ufukwe hivyo naye akatoa masharti kuwa atavipima mara tu akiruhusiwa kumiliki ufukwe. Wanzala hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Majibu ya viongozi wa wizara

Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji, Albina Burra, amesema hajui mabadiliko hayo ya ardhi.

“Mie sijui lolote kuhusu eneo hilo, sijapewa taarifa au dondoo zozote – ziwe za maneno au barua – kuhusu kubadilishwa kwa matumizi ya shamba hilo.

“Ninachoona mie ni kama wewe. Kuna mambo yanaendelea tu, naona nyumba zinajengwa na wala hakuna mchoro wowote uliopita kwangu, ili kupata majibu hebu muone Kamishna wa Ardhi, anaweza kuwa na majibu,” amesema Burra.

JAMHURI iliwasiliana na Kaimu Kamishna wa Ardhi, Bramsiden Sichone, ambaye naye alisema hana taarifa kuhusu suala hilo hadi atakapofanya utafiti na kumtaka mwandishi kuwasiliana na mtu ambaye angesaidia katika suala hilo.

Akizungumza na JAMHURI, mtumishi huyo wa wizara ambaye hakuta jina lake litajwe gazetini, amesema mgogoro huo ni mkubwa kutoka na kila kiongozi kupata kigugumizi kuushughulikia.

“Hapa hakuna kigugumizi kuzungumzia suala hili. Hii ni nchi yetu lazima tuoneshe uzalendo. Hapa kuna matatizo makubwa, hakuna kilichofanyika kule katika kupanga mipango miji kuna mambo matatu ya kufanyika.

“Kwanza unapima eneo zima, pili kujua viwanja vinakaaje na mwisho upimaji wa viwanja vyenyewe hapa hakuna kilichoafanyika.

“Sijui tunapata wapi ukakasi wa kusema hayo huyo bwana kakiuka sheria ya ardhi katika umiliki wala kubadilisha matumizi ya ardhi kinyume na sheria, kama ulivyoeleza mwanzo iko wazi kabisa.

“[Sheria inasema] watu wasio raia hawatapewa ardhi isipokuwa kupitia TIC. Si hivyo tu, hata kampuni za kigeni hawaruhusiwi kununua ardhi kutoka kwa wanakijiji bila kupata kibali kutoka TIC bali wanatakiwa kuwasiliana na Kituo cha Uwekezaji.

“Hata hawa TIC ni wateja wetu kama mteja mwingine. Wanakuja hapa na kununua ardhi kutoka kwetu, wao ndiyo wanawakodishia wawekezaji kwa muda maalumu utakaopangwa. Wakishindwa wanatakiwa kurudisha TIC,” amesema.

Amesema sheria na sera za ardhi zinatamka wazi halmashauri ina mamlaka ya kugawa ardhi hadi ukubwa wa eneo la ekari 500 ikizidi hapo ni kazi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, chini ya Kamati ya Ardhi ya Taifa inayoongozwa na Kamishna wa Ardhi Taifa.

“Ninalifahamu suala hilo, ndiyo kuna makosa makubwa, ndiyo maana umeambiwa uje kwangu kwa kuwa wanajua nalifahamu,” amesema.

JAMHURI imewasiliana na Meneja wa Amboni Beach, Steve Kabwoya, ambaye amekiri kuuza viwanja katika eneo hilo la ufukwe.

“Tumesitisha kuuza viwanja kutokana na mwanasheria wetu wa mwanzo kutudanganya kuwa tuna haki ya kuuza viwanja katika eneo hilo. Baada ya kubaini hilo tukasitisha, lakini sasa tumeamua kuwekeza katika hoteli,” amesema Kabwoya.

Amesema jambo hilo kwa sasa limesitishwa baada ya kubaini kuwa jambo hilo ni kosa kisheria. Hata hivyo, alipoulizwa ni viwanja vingapi vilivyouzwa hadi sasa katika eneo hilo, alidai kuwa swali hilo ni gumu kwa sasa na kwamba anayetakiwa kulijibu ni bosi wake Dk. Hess, aliyedai kuwa amesafiri kikazi.