Marekani itatuma msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 1.7 kwenda Ukraine.
Msaada huo unajumuisha makombora ya mifumo ya ulinzi, risasi, mabomu na aina nyingine ya vilipuzi vya kushambulia vifaru na meli za kivita.
Hayo yalielezwa na maafisa wa utawala wa Marekani. Awamu hiyo mpya ya msaada inatolewa ikiwa zimepita wiki mbili tangu kumalizika kwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO uliofanyika mjini Washington ambao nchi washirika ziliutumia kusisitiza dhamira yao ya kuendelea kuisaidia Ukraine.
Rais Joe Biden wa Marekani alitangaza wakati wa mkutano huo kwamba Washington itaipatia Ukraine mfumo wa ulinzi wa anga chapa Patriot ambao umekuwa ukiombwa kwa muda mrefu na Rais Volodymyr Zelenskyy.
Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Kirby amesema awamu hiyo mpya ya msaada utaipatia nguvu zaidi Ukraine kupambana na vikosi vya Urusi.