Na Stella Aron, JamhuriMedia, Bagamoyo
IMEELEZWA kuwa ili kupata matokeo chanya katika utunzaji mazingira na uhifadhi kuna umuhimu mkubwa wa kushirikisha sekta binafsi ambazo zimeonyesha juhudi kubwa la kuleta mabadiliko katika sekta
Hayo yalibainishwa wakati wa semina iliyoshirikisha wahariri iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa ufadhili wa mradi wa “Tuhifadhi Maliasili” unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) iliyofanyika wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi, mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga, amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa ushirikishwaji wa sekta binafsi katika ili kuleta mabadiliko kwenye uhifadhi nchini.
Alisema uchache wa wadau na wawekezaji binafsi waliopo sasa kwenye masuala ya uhifadhi na mazingira umesaidia kuimarishwa kwa shughuli za utalii na utunzaji wa shoroba za wanyamapori nchini.
” Kama sekta binafsi itashirikishwa kikamilifu na kuwekeza kwa wingi kwenye masuala ya uhifadhi na mazingira inaweza kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na watu wanaoweza kulizungumza kwa kina ni Wahariri kupitia kalamu zenu” amesema.
Amesema wanyamapori wanaopatikana katika hifadhi za Taifa na maeneo tengufu wamekuwa wakitumika katika shughuli za utalii na uwindaji na hivyo kuipatia nchi mapato ambayo yanatumika katika kuboresha huduma za kijamii, hii ina maanisha kama kutakuwa na uwekezaji mkubwa ni wazi nchi itafaidika zaidi.
“Ikiwa sekta binafsi itashirikishwa kikamilifu inaweza kuendelea kuwa na mchango katika pato la taifa ana hata kazi ya ulinzi wa misitu, hifadhi na mapori tengefu utakuwa ni mkubwa kwa sababu hakuna mtu aliyeweka hela zake atakubali kuharibu mazingira ambao utakuwa ni chanzo cha kutowesha wanyama katika eneo alilowekeza.
“Ni kweli sasa tunakabiliwa na tishio la mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaweza kutowesha viumbe pori tulivyo navyo, lakini kama sekta binafsi itashiriki kikamilifu kwenye biashara ya uhifadhi na mazingira ni wazi maeneo mengi ya hifadhi yatakuwa salama,” amesema Dk. Kalumanga.