Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ameshiriki misheni ya kuokoa zaidi ya watu 5,000 waliokumbwa na mafuriko kaskazini-magharibi mwa Korea Kaskazini, vyombo vya habari vya serikali viliripoti Jumatatu.
Mvua kubwa iliyonyesha Jumamosi ilisababisha mto kwenye mpaka wa Korea Kaskazini na Uchina kuvuka kiwango cha hatari na kusababisha “mgogoro mkubwa,” Shirika rasmi la Habari la Korea Kaskazini lilisema.
Takriban helikopta 10 za kijeshi na boti za jeshi la wanamaji na serikali ziliunganishwa kwa ajili ya juhudi za kuwahamisha waathirika katika mji wa Sinuiju na mji wa Uiju ambako mafuriko yametokea.
KCNA haikutaja vifo vyovyote au uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo. Ilisema kila moja kati ya takriban helikopta 10 ilifanya safari kadhaa ili kuwahamisha wakaazi licha ya hali mbaya ya hewa, na hatimaye kuokoa watu 4,200 walioathirika kwa ndege.