Na Irene Mark, JamhuriMedia, Morogoro

“UKISIKIA Mzazi anamwambia kijana wake ‘mleke huyo kokudanila’ hicho ni Kiluguru maana yake mwache huyo anakudanganya, hapo Mtoa Huduma za Afya ngazi ya Jamii sina cha kumwambia huyo kijana akanielewa.

…Na hiyo ilikuwa sababu ya vijana wengi kushindwa kufika kituoni kupata huduma matokeo yake anakuja dakika za mwisho ule ugonjwa umemla mpaka unataka kumaliza sehemu yenyewe.

Hapa bwana magonjwa ya zinaa hasa Kaswende ipo sana, kuna kijana alikuwa anajificha mpaka alipoanza kutoa harufu mbaya wenzake wakambana ikabidi aseme, ndio wakamleta nyumbani kwangu nikamleta kitoni akapata huduma,” anasema Mohamed Komola Mtoa Huduma ngazi ya Jamii (CHW) Kata ya Mikese Fulwe, WIlaya ya Morogoro Vijijini.

Komola anasema baada ya kuanza kwa mradi wa Afya kwa Vijana chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya, mwamko wa wazazi kuwahamasisha vijana wao kufuata elimu na huduma umekua mkubwa hali iliyopunguza kasi ya magonjwa ya zinaa.

Anasema elimu ya Afya kwa Vijana inawafikia walengwa hadi kwenye maeneo yao ‘vijiwe’ huku akisisitiza kwamba mradi huo wa Umoja wa Ulaya, umewezesha vituo kuwa na michezo mbalimbali kwa vijana ikiwemo mpira wa miguu ili kutoa elimu ya afya kwa njia ya burudani.

Mwajuma Kassim, muuguzi wa Zahanati ya Mikese Fulwe aliyepata mafunzo ya huduma rafiki kwa vijana anakiri kupungua kwa wateja wa magonjwa ya zinaa tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita.

“Mradi huu wa Afya kwa Vijana chini ya Umoja wa Ulaya ulianza hapa kwetu Oktoba, 2022 ukiangalia rejista zetu za kila siku za wateja utaona ongezeko la vijana kufika kituoni kupata elimu na huduma tofauti na awali.

Kabla ya sisi watoa huduma kupata mafunzo kwa mwezi Zahanati yetu ilirejista vijana wawili mpaka watatu kwa mwezi wanaokuja kupata huduma za afya sasa akifika tunaanza kumuelimisha umuhimu wa kutunza afya.

Baada ya sisi kupata mafunzo ya huduma rafiki kwa vijana, tumefanikiwa kupata vijana kati ya 80 mpaka 200 kwa mwezi na sisi tuliweka utaratibu wa kuwasubiri vijana wanaotoka shule hivyo kila baada ya saa za kazi anakuwepo muuguzi mwenye elimu mpaka saa 11 jioni,” anasema Mwajuma.

Kwa mujibu wa muuguzi huyo mwenye mafunzo huduma rafiki kwa vijana hata idadi ya vijana wanaokuja kwa kesi za magonjwa ya zinaa zimepungua kutoka vijana saba mpaka 18 kwa mwezi mpaka vijana wawili hadi wanne kwa mwezi.

“Vijana wengi wanaokuja kwa magonjwa ya zinaa hasa kaswende na gono ni wavulana tena wengi wanakuja kwa kuchelewa jambo linalohatarisha mgonjwa kupata ugumba baadae, wakija hapa tunawataka wawelete wenza wao,” anasema Mwajuma.

Katika maelezo yake muuguzi huyo anasema elimu ya Afya kwa Vijana imewaibua hata vijana waliokuwa wanalawitiwa ambao walifika kituoni kupata elimu ili waachane na vitendo hivyo, pia kupungua kwa wateja wa magonjwa ya zinaa na mimba za utotoni ambapo kwa mwaka huu 2024 mpaka Julai, zahanati hiyo ilipokea kesi mbili tofauti ni mwanzo kituo kilipokea mpaka kesi 11 za miamba za utotoni.

“Anakuja binti wa miaka 14 anajifungua hali ilikuwa mbaya lakini sasa kwa mwaka mmoja wa mradi huu, kesi za watoto kupata mimba zimepungua,” anasema Mwajuma.

Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Mkoa wa Morogoro, Catherine Madaha amesema mkoa huo umeshika namba tatu kati ya mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya, walifanikiwa kupeleka Mradi wa Afya kwa Vijana chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.

Anasema mradi huo umeongeza hamasa kwa vijana kati ya miaka 15-24 kufika kwenye vituo vya huduma kupata elimu na huduma kutoka kwa watoa huduma waliopata mafunzo ya huduma rafiki kwa vijana chini ya mradi huu.

“Mradi huu upo kwenye Halmashauri nne za Morogoro Vijiji, Gairo, Ulanga na Malinyi hizo ni halmashauri vinara kwenye tatizo hilo… hata hivyo takwimu zinaonesha kuongezeka kwa matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango kimkoa na kupungua kwa magonjwa ya ngono.

“Kabla ya elimu hii hali ilikuwa mbaya kwa vijana, wengi walipata mimba wasizozitarajia wakiwa watoto, ulawiti ulikuwepo magonjwa ya ngono ikiwemo kisonono, gonorea na kaswende vijana wengi waliathirika na magonjwa hayo ya zinaa.

“Yupo kijana alikuja hapa akiwa na gonorea ambayo lilimla mpaka alitaka kupoteza maumbile, wenzie walianza kumsikia anatoa harufu mbaya wenzake waka ikabidi atoe siri kwamba anaumwa wakamleta kwangu nikampa elimu nikampeleka kwa wauguzi zaidi,” anaeleza Komola.

Akifafanua zaidi anasema barabara kuu inapita hapa changamoto ni mwingiliano wa wageni na wenyeji ni mkubwa na wapo wanaoishi kwa biashara ya kuuza miili hivyo magonjwa haya yapo sana kwa vijana.

Mradi wa Afya kwa Vijana umeleta mwamko sasa wazazi wanawaleta vijana wao kituoni kupata elimu sahihi ya afya hasa afya ya uzazi.

“Hapa Morogoro kuna kesi za magonjwa yanayosababishwa na ngono isiyo salama hasa kwa vijana yapo na tunapambana nayo kupitia Halmashauri zetu chini ya Mradi wa Afya kwa Vijana unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

“…Tangu kuanza kwa mradi huu Oktoba 2022 tunaona namna magonjwa hayo yanavyopungua kwa sababu kwa mwaka huo tulipokea wateja 164 vijana wenye miaka kuanzia 15 mpaka 24 wa Kaswende na 728 wenye magonjwa mengine yatokanayo na ngono.

“Mwaka 2023 wateja vijana wenye umri huo waliofika vituoni walikuwa 141 kwa kesi ya kaswende na 591 kwa magonjwa mengine ya ngono isiyo salama.” Anasema Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Morogoro, Catherine Madaha.

“Upatikanaji rahisi wa elimu sahihi ya afya ya uzazi, usafi na matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango ndio siri ya mafanikio ya Mkoa wetu wa Morogoro kupunguza kasi ya magonjwa yanayoambukizwa kwa ngono.

Ndio, hali ilikuwa mbaya… vijana kati ya miaka 14 mpaka 23 wengi walikuwa wanapata magonjwa ya ngono kama kaswende na gonorea kwa sababu hawakujua wapi pa kwenda kupata elimu ya kuwatoa kwenye tatizo.

Oktoba 2022 baada ya Umoja wa Ulaya kutuletea Mradi wa Afya kwa Vijana, takwimu zinaonesha kupungua kwa magonjwa hayo hapa Morogoro na kuongezeka kwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango,” anasema Mratibu wa Uzazi.

“Kwa mwaka mmoja matumizi ya njia za uzazi wa mpango umeongezeka kutoka asilimia 65.1 Desemba mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 73 Desemba mwaka 2023.

“…Kwa kipindi hicho wateja wa njia za uzazi wa mpango wa muda mrefu wameongezeka kutoka asilimia 56.1 hadi 62.1 kwa kuwa mradi ulianza Oktoba sisi baseline yetu ni Desemba.

“Tunaamini mradi huu wa Afya kwa Vijana chini ya Umoja wa Ulaya utatuondoa Mkoa wa Morogoro kwenye viwango vya juu vya mimba za utotoni na magonjwa ya ngono hasa kwa vijana,” anasema Madaha.

Lailati Juma (19) kijana kinara aliyepata elimu ya Afya ya Uzazi kutoka Kata ya Mikese Fulwe mkoani Morogoro