MWANAMKE mkazi wa kijiji cha Katente wilayani Bukombe, mkoa wa Geita, Rehema Paulo (26) amejeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani, mkono wa kushoto na kutenganishwa kiganja cha mkono wa kulia chanzo kikidaiwa kuwa wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo amesema hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Geita na kueleza mtuhumiwa wa tukio hilo ni mpenzi wake anayefahamika kama Baba Lawi.

Kamanda Safia amesema tukio hilo limetokea Julai 24, 2024 usiku ambapo siku ya tukio Rehema alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu ili waende wakaonane naye akaitikia wito.

“Siku ya tukio alipigiwa simu na mtu kwamba waende wakaonane, alipomjulisha kwamba amefika ndio akavamiwa na hili tukio likatokea,”amesema Kamanda.

Kamanda amefafanua kuwa uchunguzi unaonesha mtuhumiwa ambaye ni baba Lawi ana mke mwingine ambapo wote kwa pamoja wametoroka nyumbani.

“Jeshi la polisi linaendelea kuwafuatilia ili kuwapata, tunaamini tutawapata kwa sababu taarifa tunazo za uhakika tutawakamata na sheria itafuata mkondo wake.”amesema kamanda Safia

Amewahakikishia wakazi wa Geita kutokuwa na hofu kwani ni shwari huku baadhi ya matukio yanayotokea yanasababishwa na visasi na kujichukulia sheria mkononi.

Ameongeza: “Ukiangalia huyu mwanaume hata kama ni wivu wa kimapenzi kama angefuata sheria tusingefikia hatua hii. Hatma yake Geita inaonekana haikaliki kumbe ni vitu vya watu kujichukulia sheria mkononi.”

Kamanda Safia amewasihi wananchi kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama pale panapotokea mgongano wa kifamilia na wakati mwingine washirikishe dawati la ustawi wa jamii iwapo wana msongo wa mawazo.

Please follow and like us:
Pin Share