Na Mwandishi Wetu,, JammhuriMesia, Arusha.

Serikali imeweka mazingira rafiki na thabiti kwa makundi yote katika jamii kufikiwa katika ukusanyaji maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha, Mwanazuoni na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Saikolojia Dk Richard Shukia amesema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kutoa maoni kwa wingi kwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ni mali ya wananchi siyo ya Serikali.

Aidha amepongeza idadi kubwa vijana wanaoendelea kutoa maoni yao huku akisisitiza kundi la wanawake kutambua umuhimu wa kutoa maoni yao ambayo yatasaidia kutoa muongozo wa namna nchi inapaswa kwenda.

Mmoja wa waandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Idara ya Saikolojia Dr. Richard Shukia.

“Kwa makundi maalum ya Watu wenye ulemavu, tunazingatia miundombinu rafiki ili wawasilishe maoni yao kwa ufasaha na kwa wakati, lakini pia vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha jamii kutumia nafasi hii kutoa maoni yao ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi” amesema Dr. Shukia.

Sambamba na hayo amebainisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kutokana na Dira iliyopita ambayo ni maboresho katika nyanja za afya, elimu, miundombinu ya mawasiliano pamoja na Miundombinu.

“Ukiachana na mafanikio hayo lakini pia kuna changamoto ambazo zinachangia kutokufikia kwa malengo ya Dira ya maendeleo ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi yanayopelekea mafuriko, ukame, maporomoko na maafa mengine, na mlipuko wa ugonjwa wa COVID uliochangia idadi kubwa ya watu kukosa kazi kwa wakati huo” amefafanua Dr. Shukia.

Kwa upande wake Mwandishi wa Redio Five Ashura Mohamed ametoa maoni yake juu ya maandalizi ya dira mpya ya 2050 kwamba, ni muhimu wanawake na vijana waone umuhimu wa kutoa maoni yao ili Serikali itambue nini kiongezwe na nini hakiko sawa katika suala la huduma za kijamii.

“Leo sisi ni vijana lakini miaka 25 ijayo tutakuwa wazee, hivyo tutoe maoni chanya yatakayoijenga Serikali yetu na kutupa huduma bora” amesema Ashura.

Waandishi Wa Habari wa Mkoa wa Arusha wakiwa katika semina fupi ya Uwezeshaji Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwandishi wa Habari wa Redio Safina iliyopo Jijini Arusha Willy Cosmas amesema semina aliyoipata imempa hamasa ya kutambua umuhimu wa kutoa maoni na kuhamasisha vijana wengine na jamii kwa ujumla kutoa maoni sawasawa na inavyotakiwa kama haki yao ya msingi.

“Nitaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali juu ya fursa hii muhimu ili tupate Dira nzuri 2050 itakayotupa nafasi ya kuzidi kukuza uchumi wetu kama Taifa” ameeleza Willy.

Elimu hii inaendelea kutolewa leo katika ukumbi wa AICC jijini Arusha ambapo makundi mbalimbali ya wananchi watapata nafasi ya kujadiliana na kutoa maoni yenye lengo la kuisaidia nchi kupiga hatua Katika nyanja zote za kimaendeleo.