Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameonya, binadamu wanakumbwa na janga la joto kali na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kupunguza athari za mawimbi ya joto yanayozidishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Guterres amesema kuwa mabilioni ya watu wanakabiliwa na janga hilo la joto, huku viwango vya joto vikidizi nyuzi joto 50 kote duniani.
Kwa mujibu wa mtandao unaofuatilia sayari ya dunia na mazingira yake kwa manufaa ya raia wa Ulaya wa European Copernicus, Julai 21, 22 na 23 ni siku tatu zilizokuwa na joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa duniani kote, huku Julai 22 ikishikilia rekodi kwa viwango vya nyuzi joto 17.16.
Guterres alisisitiza wito wake kwa watu kupambana na kile alichokiita uraibu wa nishati ya visukuku na kusema kwa sasa mtazamo wao ni juu ya athari za joto kali, lakini haipaswi kusahaulika kwamba kuna dalili nyingine nyingi mbaya za mgogoro wa hali ya hewa kama vile vimbunga vikali zaidi, mafuriko na ukame.