Mdau maarufu wa soka nchini, Michael Wambura (pichani kulia), amekosoa soka la Tanzania kwamba linadumazwa na uongozi mbovu.

Mtazamo wa Wambura ni kwamba kiwango cha kandanda nchini kitaendelea kushuka, kama hatua madhubuti hazitachukuliwa mapema kukabili vikwazo vilivyopo.

 

“Mpira hapa kwetu (Tanzania) haukui, unadumaa, hivyo unahitaji viongozi madhubuti kuuboresha,” anasema Wambura katika mahojiano na JAMHURI Dar es Salaam juzi.

 

Wambura aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (mwaka 2001- 2004), anasema kumekuwapo na mizengwe katika uchaguzi wa viongozi na usajili wa klabu, hali ambayo inakwaza maendeleo ya mchezo huo nchini.

 

“Angalia, kwa mfano, karibu timu 10 kati ya 14 zinazocheza Ligi Kuu zinatoka ukanda mmoja wa Pwani (akimaanisha Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani) wakati nchi inaundwa na mikoa zaidi ya 25,” anasema.

 

Anapenda kuona jitihada zaidi katika kuboresha michakato ya uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), vyama vya makocha na waamuzi nchini.

 

“Tupate viongozi wenye sifa, tupate viongozi wasio wa kikundi cha watu fulani,” anasisitiza.

Makocha wageni

Kwa upande mwingine, Wambura aliyepata pia kuwa Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (mwaka 1996-2004), ameeleza kutoridhishwa na uamuzi wa timu za Simba, Yanga na Azam kutumia makocha wa kigeni, akisema utaratibu huo unawabwetesha wazawa.

 

“Pamoja na jitihada za Rais Jakaya Kikwete kuelekeza fedha nyingi kusaidia uboreshaji wa soka nchini, kiwango cha mchezo huo hakijaridhisha,” anasema.


Hata hivyo, anatumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kutokata tamaa ya kuendelea kusimamia na kugharimia uboreshaji wa soka na michezo mingine nchini.


“Lakini pia jamii ya Watanzania itambue kwamba ina wajibu wa kuchangia kwa hali na mali maendeleo ya soka na michezo kwa ujumla nchini,” anasema Wambura.