Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe wameupongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi madhubuti wa ujenzi wa barabara ya Itoni – Lusitu kwa kiwango cha zege yenye urefu wa kilometa 50 ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Itoni -Ludewa – Manda (Km 211.4).
Barabara hiyo ni kiunganishi cha nchi za Malawi na Tanzania upande wa nyanda za juu kusini mwa Tanzania na ukikamilika utachochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa usafiri, urahisishaji wa kufanya biashara na kuwezesha wananchi kuchangamana kwa urahisi, kuwezesha kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii, kuwa kiungo kizuri kati ya mgodi wa makaa ya mawe (Mchuchuma) bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa. Pia Barabara hii ikikamilika itakuwa kiungo kizuri na barabara za ushoroba wa Makambako hadi Ruvuma.
Akizungumza mara baada ya ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM mkoani Njombe, Katibu wa CCM Mkoa wa mkoa huo Ndg Julius Peter amempongeza Rais wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo inafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ndiyo watekelezaji.
Amesema kuwa CCM imeridhishwa na ujenzi huo ambao ulisimama kutokana na mvua kubwa za El-Nino ambazo zilizokuwa zinaendelea kunyesha na baada ya mvua hizo kumalizika sasa amewasihi wakandarasi kuendelea na kazi ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe Antony Mtaka amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetibu vikwazo vya miradi mbalimbali mkoani Njombe ambapo ameridhia kuanza kwa mradi wa Mchuchuma na Liganga kwa kutoa shilingi Bilioni 15 kulipa fidia pamoja na kukubali kuanza kwa mradi mkubwa wa chuma wa Maganga-Matitu.
Vikwazo vingine vilivyotibiwa ni pamoja na kuimarisha na kujenga miundombinu ya barabara ikiwemo kutoa jumla ya shilingi Bilioni 120.9 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Itoni -Ludewa – Manda kipande cha Itoni – Lusitu kwa kiwango cha zege ambayo ni barabara yenye gharama kubwa kuliko zote Tanzania.
“Dhamira ya Mhe Rais kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha zege ndani ya muda kama ilivyokusudiwa, Pesa zipo wakandarasi wapo, tulipata changamoto ya mvua lakini kwa sasa miradi inaendelea na wananchi waanze kufuatilia fursa za uwekezaji zitakazoimarisha uchumi wao” Amekaririwa Mhe Mtaka
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa Wakala ya Barabara Tabzania (TANROADS) mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalua amesema kuwa Mkataba wa Ujenzi wa Barabara hii ulitiwa saini kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Cooperation kutoka China tarehe 29 Machi, 2022 kwa gharama ya Shilingi 120.9 pamoja na VAT.
Amesema kuwa Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi huo ni Cheil Engineering Co. Ltd ikishirikiana na kampuni ya Hana E&C Co. Ltd na ENGTEC Engineering (T) Ltd zote za Tanzania.