Msanii wa Muziki wa Taarabu Seif Kisauji ‘Babu wa Tik tok’ afungiwa kufanya kazi za Sanaa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Miezi sita na kupigwa faini ya shilingi Milioni 3.

Baraza la Sanaa la Taifa kupitia Sheria Na. 23 ya mwaka 1984 na maboresho yake ya mwaka 2019 ina mamlaka ya kusimamia maadili ya msingi kwenye sekta ya sanaa.

Mapema wiki hii  Seif Kassim Kisauji aliitwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhusiana na ukiukwaji wa maadili akiwa kama msanii aliyesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa kwa usajili Na. BST-9684-2023-2154.

Ukiukwaji huo wa maadili ni kinyume na Kanuni ya 25 (6) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2018 na Mwongozo wa Uzingatiaji wa Maadili katika Kazi za Sanaa wa Mwaka 2023.

Baada ya Baraza kujiridhisha kuwa alitenda kosa la kimaadili, limefikia maamuzi yafuatayo:-

Kumfungia kutojishughulisha kufanya kazi za sanaa ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe 22/07/2024 na kumtoza faini ya shilingi Milioni 3  kwa kutenda kosa la kimaadili..

Baraza limekwishatoa na kuzindua mwongozo wa maadili katika kazi za sanaa ambao unapatikana katika tovuti yetu www.basata.go.tz.