WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mapinduzi sekta ya umwagiliaji hivyo miradi yote aliyoahidi itatekelezwa Bashe alisema hayo akizungumza na wadau wa umwagiliaji katika uzinduzi wa mradi wa umwagiliaji katika bonde la Luiche wilayani Kigoma.

“ Utekelezaji wa miradi unaofanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji si hadithi, umelenga kuinua sekta ya kilimo cha umwagiliaji na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini”alisema  Bashe .

Waziri Bashe ameitakaTume ya Taifa ya Umwagiliaji ijipange kutekeleza miradi hiyo na wananchi wapuuze wanaowalaghai kuuza mashamba na akasema mradi katika bonde la Luiche wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 60 itanufaisha zaidi ya wakulima 9312.

“Msiuze ardhi yenu ambayo serikali inawekeza fedha zaidi ya bilioni 60 (Shilingi) kwa ajili yenu. Mkoa wa Kigoma ni mlango wa uzalishaji na mlango wa kuhudumia nchi Jirani,” alisema.

Aliongeza: “Serikali inakwenda kujenga jengo la ghorofa tatu ambalo litakuwa kitovu cha umwagiliaji katika Mkoa wa Kigoma na lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tanı 4000 pamoja na mtambo wa kuchakata mpunga”.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa alimshukuru Rais Samia Suluhu kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi wa Bonde la Luiche ambao umekuwa ukizungumzwa kutoka nchi ilipopata uhuru.

“Mradi huu ni mkubwa na utazingatia uwekaji wa miundombinu muhimu kama barabara na itazingatia kulinda vyanzo vya maji na mazingira,” alisema Mndolwa.

Alisema tume imepokea maelekezo ya serikali kuwa mradi ujumuishe ujenzi wa ghala, nyumba ya watumishi na ofisi ya umwagiliaji Mhandisi Umwagiliaji Mkoa wa Kigoma, Katuta Mustang amesema Mkoa wa Kigoma una eneo linalofaa kwa umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 147,000 na una skimu za umwagiliaji 59 na kati ya hizo skimu sita pekee ziliendelezwa.

“Mradi wa Ruiche unajumuisha ujenzi wa skimu kwa gharama ya Shilingi bilioni 40 na ujenzi wa bwawa lenye ukubwa wa mita za mraba 710,000 kwa gharama ya Shilingi bilioni 24 na ujenzi wa mifereji yenye urefu wa jumla ya kilomita 100 kutoa maji mashambani, ujenzi wa nyumba mbili za watumishi na usanifu wa jengo la umwagiliaji mkoa” alisema Katuta.

Mradi wa Luiche unajumuisha vijiji vya Kamara, Simbo, Kaseke, Nyamori, Msimba, Matiazo pamoja na Kagera. Mradi huo utakuwa na hekta 3000 zitakazomwagiliwa baada ya ujenzi kukamilika.

Please follow and like us:
Pin Share