Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kumkamata dada wa kazi aliyefahamika kwa jina la Clemensia Mirembe (19) aliyekuwa anatafutwa kwa kosa la kumchinja mtoto wa bosi wake.

Tukio hilo lilitokea Julai 17, 2024 ambapo dada huyo wa kazi alimjeruhi kwa kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni mtoto Malick Hashim (6) anayeishi eneo la Goba Kinzudi, Kinondoni ambapo baada
ya tukio mtuhumiwa alikimbia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 22, 2024 na Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema upelelezi wa tukio hilo la kikatili ulianza mara moja na jana Julai 21, 2024 saa 4:00 usiku Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo aliyekuwa mfanyakazi wa nyumba wa ndani aitwaye Clemensia Cosmas Mirembe (19) akiwa amejificha kwenye
“pagala” maeneo ya Goba Kizudi Kinondoni.

“Mtuhumiwa huyo anahojiwa kwa kina na atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kwa hatua zaidi za kisheria.

“Wito wetu Jeshi la Polisi ni kuwa pamoja na jitihada ambazo zinaendelea za kuzuia vitendo vya kihalifu tunawashauri wazazi, walezi, walimu, na jamii kwa ujumla kuwafundisha watoto kujenga tabia ya kutembea katika makundi lakini pia watoto wasikubali kuwakaribu na watu wasiowafahamu, watoto wasitumwe maeneo ambayo kwa mazingira ni hatarishi ikiwa ni pamoja na kuacha kuwatuma watoto wadogo maeneo mbalimbali nyakati za usiku,” amesema.

Aidha Muliro amesema kuwa usalama katika jiji la Dar es Salaam umeimarishwa kwenye maeneo mbalimbali na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea kushirikiana na vyombo mbalimbali vya dola na wananchi kwa ujumla ili kundeleza jitihada zake za kuzuia vitendo vya kihalifu.