Na WAF – Dar Es Salaam

Melivita ya matibabu iitwayo ‘Peace Ark’ ya Jeshi la Ukombozi la watu wa China imetoa matibabu kwa wagonjwa zaidi ya elfu 5,000 kwa siku Tano baada ya kukita nanga katika bandari ya Dar Es Salaam nchini Tanzania Julai 16, 2024 itakayotoa huduma kwa siku Saba.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Julai 21, 2024 baada ya kutembelea na kukagua utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi pamoja na kujionea aina ya huduma zinazotolewa na timu ya madaktari bingwa na bobezi wa meli ya Jeshi la Ukombozi (PLA) la Jamhuri ya Watu wa China.

“Huduma zinazotolewa na wataalamu hawa wa kichina wakishirikiana na wataalamu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni pamoja na uchunguzi, matibabu ya aina zote za magonjwa ya nje, Magonjwa ya Upasuaji na Upasuaji wa kutumia Roboti, Magonjwa ya Mifupa, Uzazi na Magonjwa ya Kinamama, kutibu kwa kutumia Tiba Asili, Magonjwa ya njia ya Chakula pamoja na huduma za wagonjwa Mahututi (ICU).

Amesema, Meli hii ilipanga kuona na kutoa huduma za kiafya kwa wagonjwa 600 lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa wananchi, wataalamu hawa wanaona wagonjwa zaidi ya elfu 1,000 kwa siku.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema meli hiyo ni hospital inayotembea ikiwa na vipimo vyote vinavyohitajika ikiwemo CT-SCAN, ULTRA SOUND pamoja na vyumba Nane vya upasua na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya ndani.

“Hii ni Hospitali inayotembea kwakweli ina vitu vyote muhimu vinavyohitajika lakini pia kuna vyumba Nane vya upasuaji, wana madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, magonjwa ya moyo, meno na huduma zote muhimu.” Amesema Waziri Ummy

“Kwakweli nimefurahi kuonana na mama aliyepata mtoto kwa kujifungua salama kwenye meli hii, hii inaonesha kuwa mahusiano ya nchi hizi Mbili yamegusa maisha ya watu na mtoto huyu amepewa jina la ‘Peace of Ark’.” Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Kiongozi wa Madaktari hao na Mkuu wa Meli hio ya Wanamaji ‘Rear Admiral’ Ndugu Yong Hong Bo amesema Meli hiyo imekita nanga katika Bandari ya Dar Es Salaam nchini Tanzania kwa lengo la kutoa huduma za matibabu ya Kiafya kwa Watanzania ikiwa ni mashirikiano ya Jeshi la nchi ya Tanzania na Jeshi la nchi la Jamhuri ya watu wa China.

Mwisho, Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kuunga Mkono kwa kutoa huduma za matibabu kwa Serikali ya Tanzania ikiwa ni muendelea wa ushirikiano wao.