Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amelizungumzia Shirika la Posta Tanzania (TPC) kama taasisi ya umma kongwe na yenye matawi nchi nzima na kulipongeza kwa ubunifu na mageuzi ya kibiashara yaliyodumisha uhai wa Shirika hilo.

Akiwa katika ziara ya kikazi katika Shirika hilo leo Julai 19, 2024 jijini Dar es Salaam, Mhandisi Mahundi amepitishwa katika mpango mkakati wa kuongeza mapato ya Shirika hilo ikiwa ni pamoja na Shirika kutoa huduma za kaunta kwa biashara za mashirika na huduma za Serikali.

“Kwenye biashara kupanda na kushuka ni kawaida, nikupongeze Postamasta Mkuu kwa ubunifu na kushikamana na watumishi wako kiutendaji na kulifanya Shirika kuwa la mfano kwa posta za nchi nyingine”, amesema Naibu Waziri huyo.

Akiwasilisha taarifa na mpango mkakati wa kuongeza mapato ya Shirika, Postamasta Mkuu, Bw. Maharage Chande amesema huduma za kaunta zinazotolewa na Shirika hilo zimesaidia kuongeza kipato cha shirika kwa kufanya mashirikiano ya kibiashara na sekta ya umma na binafsi.

Akitolea mfano mashirikiano ya kibiashara baina ya Shirika hilo na Azam Pesa yaliyofanyika hivi karibuni, Chande amesema kuwa pamoja na huduma za Azam Pesa kupatikana katika kaunta za matawi ya Shirika hilo pia zitaunganishwa na huduma za duka mtandao la Shirika hilo.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mahundi amewataka watumishi wa Shirika hilo kushirikiana na kutekeleza mpango mkakati wa Shirika kuwezesha mabadiliko na kuwa katika hali nzuri zaidi ili mashirika ya Posta ya nchi nyingine yaje zaidi kujifunza na ikiwezekana kushirikiana kibiashara.