Waziri Kilimo Hussein Bashe, ametangaza neema kwa wakulima wa Katavi na kusisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuendelea kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji.

Amesema ahadi alizozitoa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan mkoani humo ni lazima zitekelezeke hivyo serikali inaendelea na uwekezaji wa zaidi ya sh. Bilioni 55 katika kilimo cha umwagiliaji.

Waziri Bashe ametangaza neema hiyo katika kijiji cha Mwamkulu Mkoani Katavi katika hafla ya Azindua ujenzi wa Maghala mawili na kuweka jiwe la Msing ujenzi wa Ukarabati wa Skimu ya Umwagiliaji iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC).

Ametumia fursa hiyo kusifu hatua ya NIRC kwa kutekeleza miradi zaidi ya 29 mkoani humo.

Amesisitiza kuwa lengo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kuujengea uwezo mkoa wa Katavi na nchi kwa ujumla katika kuzalisha chakula cha kutosha cha kulisha ndani na nje ya nchi litafikiwa kutokana na uwekezaji huo mkubwa unaoendelea.

“Naomba kuwasilisha salamu za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambae anaahidi kuja kushiriki katika uzinduzi wa miradi mingine ya Umwagiliaji katika kata ya Mwamkulu kabla ya uchaguzi ujao.

Waziri Bashe pia amewaasa wakulima wa Mwamkulu kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji ulianzishwa kwa ajili ya kuwezesha wakulima kuchangia kufanya marekebisho ya miundo mbinu na kuchangia kujenga miundo maeneo mengine

Bashe pia amehimiza Wakulima waweze kupata haki ya kumiliki maeneo yao kisheria kwa kupatiwa hati na kwamba Maeneo ambapo serikali imewekeza lazima yalindwe

Waziri bashe amebainisha kuwa Makubaliano ya Serikali ni kujenga miundo mbinu katika hekta 27000 kwa wilaya zote mbili na kwamba imeanza na hekta 6000

“Malengo ya serikali muweze kulima mara mbili hadi mara tatu kwa mwaka,”alisema.

Bashe amebainisha kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika miundo mbinu ya umwagiliaji na kwamba pamoja na uwekezaji huo mashamba yanayowekewa miundo mbinu yataendelea kuwa mali ya wananchi.

“Kuna skimu zitafanyiwa utekelezaji ambazo ni skimu za Itenka 4500, kakese 3000,kalema zaidi ya hekta 5000 .Hekta zote 25000 zitangazwe mwaka huu,”alisema.

Alisisitiza kuwa, moja ya mipango ya serikali kuwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa ili kipindi cha kiangazi wakulima waweze kulima ipasavyo.

“Nendeni Mkajisajili.Serikali inapohitaji mjisajili mkafanye hivyo muepuke kupoteza fursa ya kupata ruzuku” alisema Bashe.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume Raymond Mndolwa,ameeleza kuwa Tume imepokea maelekezo ya waziri kuweka matoleo ya maji katika miundo mbinu ya umwagiliaji na miradi yote iliyoelekezwa na Serikali ya Rais Dk. Samia katika kilimo cha umwagiliaji nchini itatekelezwa kwa wakati.

Amesema, imefanya uwekezaji mkubwa na kutumia fedha nyingi katika kuimarisha sekta ya umwagiliaji hivyo NIRC haitakubali utekelezaji wa miradi hiyo kukwama.

“Mbali na miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji sekta ya kilimo tutahakikisha tunajenga matoleo kwa ajili ya mifugo ili kupunguza migogoro inayoendelea,”alisema.

Mapema katika kikao cha wadau Mkuu wa Mkoa wa katavi, Mwanamvua Mrindoko , amewaasa wakulima na wananchi wa kata ya Mwamkulu kutumia fursa ya ukarabati wa miundo mbinu ya umwagiliaji kushiriki katika kilimo ili kuinua kipato chao na kuepuka migogoro isiyo ya lazima, inayoweza kukwamisha juhudi za serikali kuwaletea maendeleo

Naye Mkuu wa wilaya ya Mpanda, Jamillah Yusufu ameahidi kushirikiana na viongozi wengine kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya Rais na wizara kuhusu utunzaji wa miundo mbinu na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika wilaya ya Mpanda Waziri Bashe pia ameeleza kuwa Rais ameagiza kununuliwa Pawatila zaidi ya 800 na zisambazwe kwa wakulima wadogo nchini.