Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), imeipongeza Benki ya NMB kwa kukuza Uelewa, Ufahamu na Elimu ya Bima kwa Jamii, huku ikivitaka vyombo vya habari nchini kuisaidia Serikali kuibeba kwa uzito mkubwa agenda hiyo ya kimkakati kuipeleka kwa Watanzania.

Pongezi na wito huo umetolewa leo Alhamisi Julai 18 na Naibu Kamishna wa TIRA, Bi. Khadija Said, alipokua akifungua mafunzo ya siku ya moja Huduma za Bima Mtawanyo (BankAsuarance) kwa Wahariri na Waandishi Waandamizi wa Vyombo vya Habari, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Bi. Khadija alimwakilisha Kamishna wa TIRA kufungua mafunzo hayo yaliyohusisha mada mbalimbali zikiwemo Bima ni Nini, Benki Wakala wa Bima, Kazi za NMB Katika Uwakala, pamoja na Huduma za Kibenki na Bima Rafiki kwa Wanahabari zilizotolewa na Meneja Mwandamizi wa Bima wa NMB, Martine Massawe.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Bi. Khadija alisema NMB imechukua hatua kubwa kwa kutenga muda wa kutoa elimu kwa wahariri na wanahabari waandamizi, ambao kwa kutumia vyombo vyao vya habari, wataongeza uelewa na elimu ya bima kwa jamii, ambalo ndio lengo chanya la Serikali.

“Niwapongeze NMB kwa mchango mkubwa katika kukuza uelewa wa elimu ya bima kwa jamii, inachofanya hapa ni kutekeleza Mpango Mkakati wa Serikali na Mpango Mkakati wa TIRA, unaotaka kufikia mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wawe na elimu ya bima na asilimia 50 kati ya hao wawe wanatumia Huduma za Bima.

Alibainisha ya kwamba Miongozo ya BenkiBima (BankAsuarance) imetolewa kwa mujibu wa Sheria, Kifungu cha 6(2) na Kifungu cha 11(A na B) ya Sheria ya Bima Sura ya 314, ambacho kinataka Mamlaka kuweka vigezo vya Bima vinavyopaswa kuzingatiwa na Taasisi za Fedha katika utoaji bima.

Bi. Khadija alikiri ya kwamba Benki Bima ni sekta inayokua kwa kasi nchini, ikihusisha Sekta ya Fedha na Sekta ya Bima yenyewe, siri ya ustawi na ukuaji huo sio tu suhirikiano baina ya taasisi hizo, bali pia mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kujenga na kuimarisha uelewa kwa jamii.