Na Anangisye Mwateba-Nachingwea Lindi

Wizara ya Maliasili na Utalii  inatarajia kugawa mabomu baridi yapatayo 700 kwa ajili kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu wilayani Nachingwea.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa kata za Mkoka na Kilimarondo wilayani Nachingwea, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kuwaeleza wananchi juu ya jitahada zinazifanywa na serikali kudhibiti changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.

Aidha Mhe. Kitandula alisema kuwa serikali itaendelea kutumia mbinu mbalimbali za kisayansi ikiwemo matumizi ya ndege nyuki, uvishaji wa mikanda ya mawasiliano na visukuma mawimbi, na matumizi ya helikopta katika kukabiliana na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu. Sambamba na hatua hizo, serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa askari wanyamapori wa vijiji (VGS) pamoja na kuwapatia vitendea kazi ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na hivyo kuzuia wanyama hao wasiendelee kuleta uharibifu na usumbufu kwa wananchi.

Vilevile Mhe. Kitandula alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa vijiji kuruhusu mifugo kuingia kwenye maeneo ya hifadhi vitendo ambavyo vinasababisha uharibifu wa ikolojia ya wanyama ikiwemo tembo na kuwafanya kutafuta mazingira mengine rahisi kwao kuishi.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo akimkaribisha Naibu Waziri kuongea na wananchi alisema kuwa serikali ya wilaya itaendelea kutilia mkazo suala la kuwaondoa wafugaji walioko kwenye maeneo ya hifadhi na kuwapeleka kwenye maeneo yaliyotengwa kwa kufuata Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi.

Kwa upande wake mbunge wa Nachingwea Mhe. Dr. Amandus Chinguile akiwasilisha salama za wananchi wa wilaya ya Nanchingwea alitumia fursa hiyo kuipongeza wizara pamoja na Taasisi ya Usimamizi wa wanyamapori (TAWA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), na Wakala wa huduma za Misitu (TFS) kwa kazi kubwa sana wanayoifanya ya kudhibiti ujangili wa mazao ya misitu na kupambana na wanyama wakali na waharibifu.

“Pamoja na kazi kubwa inayofanywa na askari hao lakini hawatoshi kwa kuwa makundi ya wanyama wakali na waharibifu ni makubwa, hivyo sio rahisi kwa vijana waliopo kuweza kuwamudu kwa wakati mmoja” Alisema Mhe. Chinguile.

Please follow and like us:
Pin Share