Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo wakiongozwa na kiongozi wa chama, Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita, Katibu Mkuu, Ado Shaibu na kiongozi mstaafu Zitto Kabwe wanatarajiwa kuanza ziara katika majimbo 125 yaliyopo mikoa 22 ya Tanzania kuanzia Julai 22, 2024.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Naibu Katibu wa Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Shangwe Ayo amesema Semu atatembelea majimbo 30 ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Singida na Manyara.

Amesema Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita atatembelea  majimbo 38 ya Mikoa ya Ruvuma, Mkoa wa Kichama, Selous, Mtwara, Lindi, Pwani na Tanga.

Aidha Katibu Mkuu, Ado Shaibu atafanya ziara katika majimbo 21 mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara, Geita na Kigoma.

Ayo amesema kupitia ziara hiyo ACT wanatarajia kuzindua mpango wa kusajili wanachama wapya milioni 10 kwa mwaka 2024 na 2025.

“Kwenye ziara ya ACT Wazalendo inayotarajia kuanza Julai 22, 2024 ACT Wazalendo inatarajia kusikiliza kero mbalimbali za kiuchumi, kijamii na za kisiasa za Wananchi, kuzipazia sauti na kuendelea kuinadi ahadi yake kwa Watanzania ya “Taifa la Wote, Maslahi kwa Wote,” amesema Ayo.