Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam, imeamuru Uongozi wa klabu ya Yanga ukiongozwa na Rais wake, Injinia Hersi Saidi na wenzake, kuachia ngazi na kuondoka kwenye klabu hiyo kwakuwa Katiba ya Yanga haitambui uwepo wao.

Uamuzi huu wa Mahakama umekuja baada ya Kundi la Wazee wachache waliowahi kuwa Wazee wa Yanga kipindi cha nyuma, kushitaki Mahakamani likidai uwepo wa viongozi wa sasa wa Yanga (Injinia Hersi na wenzake) ni batili na haujafuata Katiba ya klabu hiyo.

Kutokana na Wazee hao kushinda kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inamaana kuwa Rais wa Yanga Injinia Hersi na Viongozi wenzake wanatakiwa kuachia ngazi na kukabidhi Ofisi kuanzia sasa.

Kwa mujibu wa katiba ya Yanga, Injinia Hersi alitakiwa kuiongoza Yanga kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Julai 2022 alipoingia madarakani na angemaliza muda wake mwaka 2026.

Injinia Hersi alichaguliwa kuwa Rais wa klabu hiyo, mara tu baada ya kuanza kwa mfumo mpya wa mabadiliko, ambao awali nafasi za uongozi ya juu ilikuwa ni ya mwenyekiti na makamu wake.