Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

Wakazi wa kisiwa cha Utende na Chole, wilayani Mafia,Mkoani Pwani wanakwenda kunufaika na mradi wa umeme wenye msongo mkubwa wa KV 11 ,kuvuta nguzo 300 na kuzamisha waya ndani ya maji kufikisha katika visiwa hivyo.

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania( TANESCO), umetekelezwa katika sehemu tofauti kwa uwekaji wa waya wenye urefu wa kilomita 1.3 na ukubwa wa milimita 95.

Meneja wa miradi kutoka kampuni iliyopewa zabuni katika ujenzi huo, Nakuroi Investment Celestine Igongo akielezea kuhusu mradi, alieleza waya unaozamishwa ndani ya maji ambao pia unabeba nyuzi za kupitisha mawasiliano na kuwezesha mtandao kupatikana kisiwa cha Chole, una uwezo wa kubeba umeme wa msongo wa KV 33.

Alieleza ,kwa sasa umeme utakaowekwa ni wa KV 11, lakini endapo shirika hilo likiongeza uwezo wa msongo wa umeme, waya huo utaendelea kubeba umeme wa msongo mkubwa.

Igongo alifafanua, mradi huo unatarajiwa kuleta maendeleo makubwa kiuchumi kwa kutoa fursa kwa wakazi wa kisiwa cha Chole kujihusisha na shughuli zinazohitaji umeme, ikiwemo wafanyabiashara wa samaki na kuboresha utoaji wa huduma za afya.

” Mradi huu ulikuwa wa miezi Tisa, umefikia hatua za mwisho, japo tulichelewa kupata kibali cha kuvusha waya baharini, sasa tumekipata kibali tunahakikisha ndani ya wiki mbili, umeme utakuwa umewaka kisiwa cha Chole” alieleza Igongo.

Vijiji vingine ambavyo ni Juani na Jibondo, vitanufaika na upatikanaji wa umeme huo baada ya kumalizika kwa zoezi hilo katika kisiwa cha Chole.