WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kutoa masharti kwa klabu zinazomiliki viwanja vya michezo kufikia vigezo vya ubora vitakavyoainishwa na shirikisho hilo ili kufanikiwa zaidi katika sekta ya michezo na kuagiza wasiotimiza kuwekwa pembeni.
Amesema hayo leo Julai 15, 2024 katika halfa ya kuzindua mtambo wa Teknolojia ya Usaidizi wa Muamuzi kwa njia ya Video (VAR). Shughuli iliyoandaliwa na Kampuni ya Azam Media katika Viwanja vya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Kazi iliyopo TFF kuwapa masharti wanachama wao wanaomiliki viwanja asiyetimiza aweke pembeni, mukae na Azam media pamoja na wachumi ili kuingia mkataba kwa ajili ya kufanya biashara na sio siasa,
“Tunahitaji kufika mbali kwenye viwango vya Afrika baada ya namba sita basi tuwe hadi namba nne, tatu hata mbilu tukapambane na Morocco na Misri,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema Serikali imeipa michezo kipaumbele, hilo linadhihirishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuingia mwenyewe katika michezo na kuondoa ile fikra ya Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu.
“Anahamasisha kwa kutoa goli la mama kwa timu za taifa hata klabu ambazo zitashiriki michuano ya kimataifa. Pia kuwepo kwa uwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda,” amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea na maboresho ya uwanja ikiwemo miundombinu, kama uboreshaji wa viti vya mashabiki, taa za uwanjani pamoja na sehemu ya kuchezea yenye kukidhi matakwa ya TFF na Bodi ya Ligi (TPLB).
“Hii VAR inatusaidia kuondoa malalamiko kwa timu pamoja na kupunguza makosa ya kibinadamu kwa waamuzi wetu na kuwa makini katika kazi zao,” amesema Waziri Majaliwa na kuongeza kuwa
Serikali imetimiza ahadi ya waziri aliyepita katika Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa juu ya kuleta VAR,” pia Waziri Mkuu ameaiagiza wizara husika kusimamia miradi hiyo sambamba na kuongeza nguvu zaidi.
VAR ilianza kutumiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016 katika mechi za majaribio na baadaye katika Kombe la Dunia la Klabu mwaka huo.
VAR ilianza kutumika rasmi katika mashindano makubwa kama Ligi Kuu ya England (Premier League) na Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) msimu wa 2019-2020.
Katika Kombe la Dunia la FIFA, VAR ilitumiwa kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia la 2018 nchini Urusi.