Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Samia Hassan ameutangaza mkoa wa Katavi kuwa kanda maalum ya ununuzi wa mazao na uhifadhi wa nafaka ya chakula.
Ametoa kauli mara baada ya kuzindua vihenge vya kisasa, na ghala za kuhifadhia nafaka kwa msimu wa mwaka 2024/2025 katika wakala wa uhifadhi wa chakula nchini (NFRA) mjini Mpanda.
Rais Samia amewataka vijana kujihusisha zaidi na kilimo cha tija na biashara ya ununuzi wa mazao ili kutumia fursa za kuuza mazao kwa nchi jirani na kukuza uchumi.
“Tanzania ina fursa kubwa ya kuuza mazao nchi za jirani kutokana na kukabiliwa na ukame” alisema.
Awali akizindua jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Rais Dokta Samia amelitaka jeshi hilo kuendelea kuimarisha ulinzi hasa katika maeneo ya mipaka na nchi nyingine.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Hamad Masauni amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya askari.