Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu kutumia vyombo vya ulinzi na usalama alivyonavyo kuchunguza malalamiko ya akina mama wajawazito kuombwa rushwa katika Kituo cha Afya Makere kilichopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
Dkt. Mpango ametoa maelekezo hayo kwa mkuu wa Wilaya huyo, akiwa katika mji wa Makere wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma mara baada ya kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya vitendo vya baadhi ya watumishi wa kituo hicho cha Afya cha Makere kuomba rushwa ili kuwapatia huduma.
“Mhe. Mkuu wa Wilaya una vyombo vinavyohusika na uchunguzi, hivyo unaposikia malalamiko ya wananchi elekeza vyombo vifanye uchunguzi ili uchukue hatua stahiki kwa watakaobainika, lakini msiwaonee watu,” Dkt. Mpango amesisitiza.
Awali, akieleza changamoto wanazokabiliana nazo, Bi. Eva Moshi mmoja wa wananchi aliyepewa fursa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kuzungumza changamoto zinazowakabili amesema kuwa, mjamzito akienda kujifungua katika Kituo cha Afya Makere kama hana 50,000/= hatopata kadi ya kliniki na atajifungulia nje.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Zainab Katimba alipopewa nafasi ya kuzungumza amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itachukua hatua za kinidhamu dhidi ya mtumishi yeyote atakaebainika kumtoza mama mjamzito faini ya shilingi 50,000/= kwa kisingizio cha mama huyo kushindwa kufika kwa wakati katika kituo cha afya na zahanati.
“Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, ninatoa maelekezo kwa watumishi wote wa kada ya afya kutimiza wajibu wao kikamilifu na kwa wale watakaoainika kuomba rushwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mke wa Makamu wa Rais, Mama Mbonimpaye Mpango amemshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Zainab Katimba kwa kuahidi kutatua changamoto zinzawakabili wananchi na kuwapongeza wananchi hao kwa kusema hadharani changamoto wanazokabiliana nazo ili zitatuliwe na mamlaka husika.
Makamu wa Rais Dkt Mpango yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi.