WILAYA ya Kisarawe iliyoko Mkoa wa Pwani, imewaita Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), kutoa elimu kuhusiana na ufugaji kwa wana Kisarawe ili wafuge kisasa.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Petro Magoti ametoa wito huo alipotembelea banda la TVLA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

“Wilaya ya Kisarawe imekusudia kuanzisha vikundi vya wafugaji ili kuweza kuinua uchumi wa wananchi wetu. Lakini wafugaji wetu bado hawana elimu. Naomba mje kutoa elimu kwa wafugaji wetu,”amesema.

Ng’ombe

Kwa upande wake Mtafiti wa Ifugo wa wakala hao, Dk Fredy Makoga amemweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa kuchanja mifugo ni njia yenye gharama nafuu ya kudhibiti magonjwa ya mifugo.

Soma: Mifugo kufugwa, kulishwa kisasa

Amesema wafugaji wanapasa kuepuka kutibu mifugo yao kiholela badala yake watumie huduma za maabara na ushauri wa wakala huo.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania katika kutekeleza kazi zake kutokana na malengo ya kuundwa kwake ina majukumu kadhaa inayoyatekeleza ambayo ni pamoja na uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo na uhakiki wa Ubora wa Vyakula vya Mifugo.

Majukumu meingine ni usajili na uthibiti wa ubora wa viuatilifu vya mifugo, utafiti wa magonjwa ya wanyama na wadudu waenezao magonjwa hayo na kutoa huduma za ushauri na mafunzo.

TVLA ni mojawapo ya taasisis tano za sekta ya mifugo zilizo chini ya Wizara ya Mifugo.

Nyingine ni Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania(TALIRI), Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo(LITA), Bodi ya Maziwa Tanzania(TDB) na Bodi ya Nyama.

Kwa mujibu wa Sera ya Mifugo ya Julai 2020 utoaji wa huduma bora za utabibu wa mifugo sharti uzingatie viwango, maazimio na miongozo mbalimbali vya Shirika la Afya ya Wanyama Ulimwenguni (OIE) kuhusu afya na udhibiti wa magonjwa ya wanyama na biashara yake kimataifa.

Biashara ya mifugo na mazao yake inaongozwa na makubaliano ya kimataifa ya ukaguzi wa afya ya wanyama na mimea (Sanitary and Phytosanitary – SPS) chini ya Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO).

Huduma za utabibu wa wanyama hujumuisha afya, ya mifugo, udhibiti na utokomezaji wa magonjwa ya mlipuko; wadudu na magonjwa yaenezwayo na wadudu; magonjwa mengine ya mifugo yenye athari za kiuchumi; ukaguzi wa mifugo na mazao yake; afya ya jamii kuhusiana na mifugo na usalama wa vyakula vitokanavyo na mifugo.

Please follow and like us:
Pin Share