Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Serikali Mtandao (eGA) imetoa wito kwa wananchi kutumia mfumo wa e-mrejesho katika kuwasiliana na serikali kutoa hoja zao ili iweze kuzifanyia kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la eGA kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba, Meneja Mawasiliano wa eGA, Subira Kaswaga amesema suala la kujenga mifumo kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi katika utumishi wa umma ni jukumu la eGA.

“Katika jukumu hilo imejengwa mfumo wa e-mrejesho ambao ni daraja la mawasiliano ya wananchi na Serikali. Kupitia mfumo huo, wananchi wanaweza kuelezea kero,changamoto yoyote ,maoni ,kuuliza swali lolote au hata kuongeza Serikali na yote kwa pamoja yatafanyiwa kazi na Serikali.

“Mfumo unapatikana kwa njia ya simu ya mkononi kwa kubonyeza 15200# halafu namba 9 na kuendelea kufuata maelekezo na taasisi zote za Umma zimeunganishwa katika mfumo huu wa e-mrejesho, kwahiyo mwananchi akiwa na kero mbalimbali anaweza kuwasiliana na Serikali ikazifanyia kazi,” amesema Kaswaga.

Kwa mujibu wa Kaswaga huduma hiyo inapatikana kwa kupakua app ya e-mrejesho au kwa kutumia tovuti ya www.emrejesho.co.go.tz.

Aidha amesema kutokana na utendaji wake, mfumo huo umetambuliwa kimataifa kwamba ni jukwaa huru ambalo linawasaidia wananchi kuwasiliana na serikali na kupitia mfumo huo eva inaweza kushindwa tuzo katika Umoja wa Mataifa ya ubunifu wa huduma za umma mwaka huu 2024 ambazo zilitolewa nchini Korea.

Amesema taasisi hiyo pia imejenga mfumo wa kubadilishana taarifa serikalini kwa maana ya mifumo kusoma kwa lengo la kurahisisha na kuboresha uwajibikaji seeikalini.

“Kama tunavyofahamu kwamba Rais Dkt . Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza taasisi za umma kubadilishana taarifa kidigiti, kwa hiyo sisi kama mamlaka tumetengeneza mfumo huo na tayari tumeshaunganisha mifumo mbalimbali na sasa wanachokifanya ni kuzihamasisha taasisi za umma ziweze kujiunga na mfumo huo ili ziweze kubadilishana taarifa,” amesema.

Kwa mujibu wa Kaswaga mpaka sasa taasisi ambazo zimeunganishwa na mfumo huu ni taasisi 141 na mifumo 148 imeshaunganishwa na katika hiyo mifumo 109 inasomana na kubadilishana taarifa.

“Kwa hiyo tunafanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na ofisi za umma kuziunganisha kwenye mfumo huo na Julai 22 hadi 29, Mwaka huu tunatarajia kuwa na kikao na taasisi za umma taktiban 70 kwa lengo la kuwapa elimu kuhusiana na mfumo huo lakini pia kuunganisha ili hizo taasisi zijiunge na mfumo huo wa kubadilishana taarifa,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share