Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema kuwa wamejiwekea malengo ifikapo mwaka 2034, matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi yafikie asilimia 80.

Wamesema wanaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuwezesha jambo hilo liwezekane kwa kuzalisha kiasi cha gesi ambacho kitaweza kuhudumia majumbani, katika magari, na kwenye maeneo mengine.

Mhandisi Sangweni ameyasema hayo alipotembelea banda la PURA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa.

Amesema kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi unaoendelea nchini, wananchi wanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua Mazingira.

“Umefika wakati sasa wa kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira kama mkaa na kuni, na badala yake kutumia nishati safi ambayo haina madhara makubwa kwa mazingira. Kwahiyo tumeweka malengo ya kutumia nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034,” amesema.

Amefafanua kuwa, kwa sasa maeneo ambayo tayari yamegunduliwa kuwa na gesi ni pamoja na Mnazi Bay na Songosongo iliyopo Mtwara.

Ameongeza kuwa maeneo yenye viashiria vya mafuta yanajumuisha zaidi ya asilimia 50 ya eneo la Tanzania, ambapo tafiti zimefanyika katika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 160,200, hasa katika maeneo ya Pwani.

Ameyataja maeneo hayo ni Tanga, Kusini, na Mtwara, ambapo tafiti zimefanyika hadi baharini zaidi ya kilomita 400. Eneo hili tayari limepata kibali kutoka Umoja wa Mataifa (UN) na limeshagawanywa katika vitalu kwa ajili ya uwekezaji.

“Shirika linaendelea na ugunduzi katika maeneo ambayo yana viashiria vya gesi ambapo imebainika kuwa ni asilimia 50 ya eneo la Tanzania. Kwa sasa tunatangaza maeneo mbalimbali ambayo yanavutia wawekezaji kwa ajili ya kushirikiana na taasisi pamoja na TPDC katika kutafuta na kuendeleza kinachopatikana,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share