Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema watu zaidi ya 200 wameungashiwa huduma ya ‘Faiba Mlangoni’ katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya TTCL (T-Pesa), Lulu Mkudde, alipotembelea katika banda lao lililopo katika maonesho hayo.

“Huduma ya Faiba Mlangoni, ina umuhimu mkubwa kwa mteja kwani itamwongezea uwezo wa kutumia intaneti kwa haraka na ubora zaidi. Tunawahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizi za kidigitali ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani,” amesema Mkudde.

Amesema kupitia maonesho hayo, TTCL imepata fursa ya kutoa elimu na kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu huduma wanazozitoa ambazo zinawafikia moja kwa moja.

Aidha amesema hadi sasa Shirika hilo limesambaza Mkongo wa Taifa katika mikoa yote nchini, ambapo zaidi ya wilaya 98 zimeunganishwa na mkongo huo wa mawasiliano.

Amesema Shirika linaendelea na mchakato wa kufikisha huduma zake za Mkongo wa Taifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni muendelezo wa kupeleka huduma hiyo kwa nchi za jirani.

“Hadi sasa, huduma hii ya Mkongo wa Taifa imewafikishwa katika nchi nne, ikiwemo Burundi, Rwanda, Zambia, na Malawi,” amesema Mkudde.

Amesema kuwa lengo la kufungua milango ya kidigitali ni kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kutumia huduma za Interneti katika kutekeleza huduma mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu huduma ya (T-Cafe), Mkudde amesema ni huduma ya WiFi inayowaondolea adha wafanyabiashara, waandishi wa habari, na wataalamu wa ushauri katika kufanya kazi zao wakiwa nje ya ofisi.

“Huduma hii inasaidia mtu yeyote kufanya kazi nje ya ofisi kwa kutumia Interneti kwa haraka na gharama nafuu. Katika kipindi hiki cha Sabasaba, tumeona jinsi huduma hii inavyofanya kazi kwa kasi ya hali ya juu na wananchi wameitumia sana katika maonesho hayo,” amesema.