Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MKUU wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Tinda Lwoga amesema mabadiliko ya kiteknolojia yamechangia wao kuanzisha kwa kozi za Shahada ya Uzamili (Master’s) kwa njia ya mtandao.

Ameyasema hayo alipotembelea banda lao lililopo katika Viwanja vya maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.

Amesema wameanza Program hiyo tangu Machi mwaka huu kwa kutoa program zaidi ya 10 kwenye maeneo ya Biashara, rasilimali watu, masoko, benki na fedha, pamoja na Tehama.

“CBE tulianza hizo program Mwezi Machi ambapo wanafunzi wamekuwa wakishiriki hata kama yuko nyumbani, kazini, Dar es Salaam, Dodoma au Mwanza lakini anashiriki masomo yake kwenye upande wa mitihani ndo anakuja kwenye kampasi zetu.

“Kwahiyo imesaidia sana kusambaza elimu yetu ya biashara ndani na nje ya Tanzania lakini pia imeleta urahisi wa gharama mwanafunzi ahitaji tena kulipia usafiri au gharama ya malazi,” amesema.

Aidha amesema kila mwaka wanafanya kongamano la kimataifa kwa lengo la kuonyesha matokeo ya tafiti walizofanya na kuzipeleka katika mamlaka za serikali ili matokeo hayo yaweze kutumika.

Amesema pia wamekuwa wakitoa mafunzo ya muda mfupi kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kwa lengo la kusambaza matokeo ya tafiti ili waweze kuyatumia kuboresha biashara zao.

“Mwaka huu pia tumeanza midahalo ya wazi ambapo tunashirikisha wataalam mbalimbali kutoka ndani na nje ya chuo, tunaelimisha jamii kutokana na matokeo ya tafiti tulizofanya kuhakikisha Watanzania wote wanapata fursa ya kuyasikia na kuyatumia kutatua changamoto walizonazo,” amesema.

Ameongeza kuwa katika maonesho ya Sabasaba wanaonyesha huduma za elimu wanazozitoa ambapo wana mafunzo ya muda mrefu kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamili kwenye maeneo ya biashara, rasilimali watu, masoko, benki na fedha, utawala na Tehama.

Please follow and like us:
Pin Share