Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli na Gesi Asilia (PURA), Halfani Halfani ametoa wito kwa Watanzania na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika Duru ya kutangaza maeneo ya uwekezaji wa petroli na gesi nchini.
Ameyasema hayo alipotembelea banda lao lililopo katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.
Amesema PURA wamejipanga kuongeza wawekezaji kwasababu kwa kipindi kirefu hawakuwa na wawekezaji wa kutosha.
Amesema sheria ya mafuta inasema wawekezaji watafutwe kwa ushindani hivyo wanafanya mkutano wa kutangaza maeneo ya wawekezaji kuyachagua ili kutaka kuwekeza.
“Sheria ya mafuta inasema wawekezaji watafutwe kwa njia ya ushindani na sio kwa kuokotwa na ili uwapate kwa ushindani kuna kitu kinafanyika kinaitwa Duru, Duru ni mkutano wa kutangaza maeneo husika ya miradi hivyo wanakuja pale kisha wanapewa utaratibu wa kuandika madokezo ya kuomba miradi.
“Na Duru hiyo inaweza kufanyika labda robo ya mwaka ujao na duru inakuwaje ukisoma Sheria ya mafuta ni kazi ya Waziri kutoa leseni na Waziri akialikwa pale atakuja kumwaga sera na kuainisha huduma inayotolewa,” amesema.
Kuhusu miradi iliyopo amesema wanaongeza wawekezaji kwasababu kwa kipindi kirefu hawakuwa na wawekezaji au maeneo mengi walikuwapo lakini maeneo yamerudishwa serikali.
Amesema sheria ya mafuta inasema wawekezaji watafutwe kwa ushindani hivyo wanafanya mkutano wa kutangaza maeneo ya wawekezaji kuyachagua ili kutaka kuwekeza.
Aidha, amesema mkoani Mtwara amepatikana mwekezaji mpya wa uchimbaji wa gesi asilia atakayezalisha futi za ujazo milioni 100 kwa siku.
Amesema wanatarajia kiwango hicho kuongezeka na kitasaidia upatikanaji wa gesi ya uhakika.
Amesema kwa kipindi kirefu wametegemea gesi ya baharini hivyo waamini gesi hiyo itakuwa mpango madhubuti.
Amesema maeneo ya Songosongo Kilwa na Mnazibay Lindi pia wanazalisha futi za ujazo milioni 250 kwa siku na kiasi kikubwa kinatumiwa kuzalisha umeme.
“Asilimia 50 ye gesi hii inazalishia umeme na kiasi kingine minatumika kwenye matumizi mengine,” amesema Halfani.
Kuhusu majukumu ya PURA amesema ni kumshauri Waziri wa Nishati masuala ya mkondo wa juu wa utafutaji, uzalishaji na usambazaji wa gesi nchini.
Amesema jukumu la pili ni kusimamia ufanisi wa juu wa sekta kuhusu utafutaji gesi ili kujua gharama za utafutaji na wapi.
Ameongeza kuwa pia wana jukumu la kuhakikisha Watanzania wanashiriki kwenye jukumu la utafutaji na uzalishaji wa gesi.
“PURA pia ina jukumu la kutunga sera ndogo za kuhakikisha utendaji kazi unakuwa wa ufaniisi lakini pia wanasimamia uuzaji wa gesi nje ya nchi,” amesema.