Na Isri Mohamed
Watuhumiwa tisa wa mauaji ya mtoto mwenye Ualbino, Asimwe Novart wamefikishwa tena katika mahakama ya hakimu mkazi Bukoba leo Julai 12, 2024 kwa ajili ya kutajwa mashtaka yao ambapo baadhi yao wameonekana wakimwaga machozi.
“Serikali bado inaendelea na taratibu za kusajili shauri hilo katika Mahakama Kuu ambayo ndio yenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la mauaji ya kukusudia na uchunguzi wa shauri hilo no. 17740 la mwaka 2024 tayari umekamilika” amesema Wakili wa serikali, Erick Mabagala.
Kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba kukosa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ambayo shauri lake limetajwa mbele ya Hakimu Elipokea Yona Wilson, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na tayari wamerudishwa rumande mpaka Julai 26, 2024, kesi yao itakapotajwa tena huku wakiendelea kusubiri kukamilishwa kwa jalada lao.
Watuhumiwa hao tisa ni Elpidius Alfred Rwegoshora (49) ambaye ni Padri, Novart Venant (24) ambaye ni Baba mzazi wa Asimwe, Nurdin Ahmada, Ramadhan Selestine, Rwenyagira Alphonce, Dastan Buchard, Faswiu Athuman, Gozibert Arikad na Dezdery Everigis
Miongoni mwa watuhumiwa hao,mshitakiwa namba moja ambaye ni Padri Elpidius Rwegoshora tayari ameweka wakili wa kumtetea ambaye anaitwa Mathias Rweyemamu.