Urusi imekosoa mpango wa Marekani wa kupeleka makombora ya masafa marefu nchini Ujerumani ikisema hatua hiyo inawarejesha kwenye zama za Vita Baridi.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov ameishutumu Ujerumani, Marekani, Ufaransa na Uingereza kwa kujiingiiza moja kwa moja kwenye vita vyao dhidi ya Ukraine, na kusema mazingira kama hayo ndiyo yaliyovichochea Vita Baridi.
Amesema, Urusi inachukulia kwa umakini kila linalofanywa kwa lengo la kuwadidimiza na kuongeza kuwa huu ni wakati kwa wao kuungana na kutumia utajiri walionao kutimiza malengo waliojiwekea katika operesheni yao ya kijeshi nchini Ukraine.
Pembezoni mwa mkutano wa kilele wa NATO Ikulu ya Marekani pamoja na Ujerumani walitangaza mpango huo, ambao ni wa kwanza tangu kumalizika Vita Baridi.