Mwigizaji na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu amesema kuna haja ya wasanii kurudi shuleni, ili kuongeza ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kuboresha kazi zao za filamu.

Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufikiria kufanya mabadiliko makubwa katika sekta hiyo na kuwapa nafasi wasanii kwenda kwenye mafunzo na kuahidi hawatamuangusha.

Katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuzungumzia safari yao ya Korea Kusini, Wema amesema suala la elimu linahitajika kwa watu wote wanaohusika kwenye uigizaji kwa kuwa itawasaidia kufanya kazi kitaalamu na sio kubahatisha.

“Watu wasifanye kazi kwa uzoefu tunahitajika kurudi shule namaanisha wasanii, wahariri, waandishi wa hadithi, waongozaji, naamini kuna kozi mbalimbali zinaweza kutusaidia na mama atatusaidia,”amesema.

Kauli hiyo inakuja baada ya kundi la pili la wasanii kutoka Korea Kusini kwenda kwenye mafunzo na kujionea namna wenzao walivyopiga hatua kubwa, akisema hata wao wanayo nafasi ya kubadilika kutokana na kile walichojifunza.

Mbali na hilo, amesema wanahitaji kupata eneo kubwa lisilopungua ekari 200 kwa ajili ya kufanya shughuli zao za sanaa, ambalo kutakuwa na kila kitu kwa maana ya vifaa vyote muhimu vitakavyohitajika kuandaa kazi zao za filamu.