Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesisitiza umuhimu wa wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kuwasaidia wananchi kwa kutoa elimu kuepukana na maradhi mbalimbali.

Ametoa wito huo mara baada ya kutembelea Zahanati ya Kijiji cha Kasumo akiwa wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Amesema maradhi yanayotajwa kuwasumbua wananchi wa kijiji hicho ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na yanayokana na matumizi ya maji yasio salama yanaweza kudhibitiwa kwa kutoa elimu kupitia mikutano mbalimbali ya kijiji.

Amewahimiza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuwatembelea wanakijiji katika maeneo yao na kuwaelimisha namna ya kuwalinda watoto dhidi ya michezo katika maji machafu pamoja na unywaji maji yasiochemshwa.

Amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuweka utaratibu wa kuchemsha maji kabla ya kunywa na kuondokana na imani waliyonayo kwamba maji ya kuchemsha sio matamu.

Makamu wa Rais amewapongeza wanakijiji hao kwa kwa kujitoa katika kukamilisha zahanati hiyo ambayo imekua msaada kwa wananchi wa Kijiji hicho na vijiji Jirani.

Amewasihi wananchi wa Kijiji hicho kuendelea kujitolea na kushirikiana katika shughuli za maendeleo ili kuboresha maisha yao kwa vizazi vya sasa na baadae. Aidha ametoa wito kwa wanakijiji hao kuanzisha nguvu mpya ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika zahanati hiyo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekagua shuguli za maendeleo katika Wilaya ya  Buhingwe  ikiwemo ujenzi wa Shule ya Sekondari Kahimba pamoja na ujenzi wa barabara kiwango cha lami ya Muyama – Kasumo – Kabanga.

Amewataka wakandarasi kuhakikisha wanaongeza kasi katika ujenzi wa barabara hiyo wakati huu wa kiangazi ili ikamilike kwa wakati na kufungua shughuli za kiuchumi na kijamii katika Wilaya hiyo na maeneo Jirani.

Makamu wa Rais amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itakamilisha miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Kigoma ili kuvutia zaidi uwekezaji na kurahisisha shughuli za ufanyaji biashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii  Januari 31, 2024 Dar es Salaam Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema wahudumu hao ndio Mstari wa mbele katika Sekta ya Afya wanaoweza kuibua wagonjwa na kutoa taarifa zote kuhusu masuala ya Magonjwa ikiwemo yasiyoambukiza na yakuambukiza kama ya milipuko.

”Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ndio askari wa mbele katika Sekta ya Afya na ndio wanaibua wagonjwa na wanaweza wakazuia na kutoa taarifa zote kuhusu masuala ya magonjwa na ni nguzo muhimu katika kuimarisha mifumo ya Afya ngazi ya jamii ili kufikia lengo la huduma za Afya kwa wote.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy alisema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wanaenda kuwapunguzia mzigo watumishi katika ngazi za Hospitali kwa kuwa kuna baadhi ya vijiji havina vituo vya Afya au vinapatikana mbali na makazi ya watu.

“Ndio maana tumeona ni muhimu sasa turasimishe mpango huu ili kutomuacha mtu yoyote, Mfano kwa upande wa ugonjwa wa Kifua Kikuu tulipoamua kutumia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii wameibua wagonjwa wapya asilimia 50 kwa kila wagonjwa wapya 100 wanaogunduliwa na ugonjwa huo.” Amesema Waziri Ummy

Please follow and like us:
Pin Share