”UBALOZI WA UFARANSA KUADHIMISHA SIKUKUU YA JULAI 14 ,LEO HII”

Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kihistoria Tarehe ya Julai 14 ya mwaka 1789 inabaki kuwa tarehe muhimu zaidi katika historia ya mambo ya kisiasa mlnchini Ufaransa. Kwa mujibu wa historia inatueleza kuwa mnamo tarehe 14 Julai inakumbukwa kama tarehe ya mapinduzi ya kisiasa nchini Ufaransa.

Tukio kubwa la siku hii ni pale raia wenye hasira Kali kutoka katika viunga vya Faubourg Saint-Antoine huko nchini Ufaransa wakiongozwa na viongozi wa mapinduzi walipoamua kuvamia Ngome ya BASTILLE kufanya mageuzi kufuatia mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na kisiasa pamoja na utawala wa mabavu uliokuwa ukiendelea katika taifa la Ufaransa chini mfalme wa taifa hilo kwa wakati huo Mfalme LOUIS XVI(Louis wa kumi na sita) .

BASTILLE ilikuwa ni ngome muhimu na gereza lililokuwa likipatikana katikati mwa mji wa Paris ambalo lilisimama kama alama ya utawala wa kidhalimu na pia lilitumika kuwashikilia wakosoaji wa kisiasa kwa Wakati huo.

Tukio hilo lilikuwa maarufu mara baada ya waandamanaji hao kufanikiwa kuvamia Ngome hiyo na kushuhudiwa ukatili wa kunyongwa kwa Mfalme LOUIS XVI pamoja na mkewe Malkia MARIA ANTOINETTE na hatimae kufanikiwa kuumaliza rasmi mfumo wa Uongozi wa kifalme(MONARCHY LEADERSHIP SYSTEM).

Ndani ya miezi mitano baadae Gereza la Bastile lilivunjiliwa mbali na kuwekwa kwa sanamu ikiwa kama kumbukumbu ya eneo hilo. Mnamo tarehe 14 julai 1790 mwaka mmoja mara baada ya tukio la uvamizi wa Gereza la Bastille iliendeshwa sikukuu ya mashirikisho iliyofanyika katika maeneo ya Champ-de Mars ikiwa na lengo la kusheherekea mwaka moja wa uhuru wao pamoja na kuzindua enzi mpya za uongozi ambapo maelfu ya wafaransa walihudhuria hafla hiyo.

Katika miaka iliyofuatia sherehe hizo zilianza kupungua na kufifia taratibu. Hata hivyo Julai 6 ya mwaka 1880 ,Bunge la Ufaransa lilitunga sheria muhimu ilyoweka JULAI 14 kuwa sikukuu ya kitaifa kwa Jamhuri ya Ufaransa. Katika siku hiyo jamii ya wafaransa wanasherekea alama zote kuu zinazowakilisha taifa lao kama vile bendera ya taifa yenye rangi tatu na wimbo wa taifa ambavyo vyote chimbuko lake ni mapinduzi yaliyoitwa mapinduzi ya BASTILLE.

Mpaka kufikia miaka ya hivi karibuni huko nchini Ufaransa tarehe 14 Julai inajulikana kama Sikukuu ya kitaifa ambayo wafaransa huiita (FĂȘte Nationale) kwa lugha ya kifaransa na huadhimishwa kwa Sherehe za Kitaifa ambazo hufanyika katikati mwa mji wa Paris. Sherehe hizo zinajulikana Kama (Quatorze Juillet) kwa lugha ya kifaransa.

Sherehe hizo hufanyika kila ifikapo julai 14 huko mjini Paris,Ufaransa. Kitamaduni siku hii huambatana na matukio mbalimbali yakiwemo Gwaride la kijeshi, kupigwa kwa mafataki ya moto angani, mjumuiko wa watu katika hafla ya kula na kunywa pamoja na kudumisha Upendo na usawa kwa kila raia wa taifa hilo.

Hapa nchini sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika leo hii katika makazi rasmi ya Balozi wa Ufaransa na kuongozwa na Balozi wa Serikali ya Ufaransa hapa nchini MH; Nabil Hajlaoui ambapo atajumuika na raia wengine wa Ufaransa waishio hapa nchini pamoja wageni waalikwa ikiwa ni kudumisha tamaduni ya siku hiyo ya kitaifa ya taifa la Ufaransa.

Wajuzi wa Mambo ya kisiasa wanaielezea vyema siku hii kama siku ya Taifa la Ufaransa kwa kile wanachoamini tukio la JULAI 14 ndilo lilitengeneza taswira mpya katika mfumo wa Uongozi nchini Ufaransa..