Nimefanya naye kazi kwa karibu kuanzia Mei 28 hadi Novemba 3, 2007 na kisha Septemba 30, 2009 hadi Septemba 24, 2010.

Nilipohamia Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Dar es Salaam, nikitokea mkoani Kilimanjaro nilikokuwa Katibu Msaidizi wa CCM wa Wilaya ya Moshi Mjini, Amos Gabriel Makalla (41) alikuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo.

Aliniacha hapo alipoteuliwa kuwa Mweka Hazina Mkuu wa CCM Novemba 3, 2007. Lakini nikaungana naye tena Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM jijini Dar es Salaam nilipohamishiwa hapo Idara ya Itikadi na Uenezi Septemba 30.

Nilifanya naye kazi tena hadi Septemba 24, 2010 nilipoteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Iringa Mjini, nafasi niliyoitumikia hadi Agosti 18, mwaka jana.

Katika hali hiyo, naujua kwa kiwango kikubwa uzuri na ubaya wa Makalla ambaye siku 12 zilizopita, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, wiki iliyopita, Ikulu Dar es Salaam.

Uzuri mmojawapo wa Makalla ni kutokubali kushindwa anapoamua jambo lake hata kama wengine hawawezi hata kulifikiria pekee.

Inawezekana upambanaji wake, uchapakazi wake, uamuzi wake mgumu na mengine yakiwa ya hatari, uwezo wa utendaji, ubunifu wake, utashi wake na kiwango cha uthubutu, ndivyo vilichangia kupanda ngazi kwa haraka – yakiwamo madaraka ya kuchaguliwa – akatoka ‘chini kabisa hadi juu kabisa’ kwa miaka minne tu.

Baadhi ya uamuzi mgumu aliowahi kuufanya ni kuacha kazi kwa notisi ya saa 24 tu kwenye Kiwanda cha Matofali cha Kisarawe mkoani Pwani. Alitakiwa achague moja kati ya utumishi ama aondoke alipogundulika kuwa anajihusisha na siasa wakati mwajiri wake hataki.

Pamoja na kutokuwa na kazi nyingine wala tegemeo la kupata ajira na akiwa hajui angeishi vipi na familia yake, Makalla aliacha kazi akiwa Mhasibu Mwandamizi wa Kiwanda hicho na kurejea nyumbani kwake Kawe, Dar es Salaam. Ilikuwa mwaka 2003.

Akiwa amebaki tu kuwa Mwenyekiti wa UVCCM wa Kata ya Kawe, wadhifa alioupata kwa kuchaguliwa mwaka 1999 lakini ikiwa ni kazi ya kujitolea isiyokuwa ya mshahara, baada ya kusota kijiweni kwa miezi kadhaa, aliajiriwa na taasisi hiyo ya CCM na kuteuliwa kuwa Katibu wa Usalama na Maadili.

Alipanda ngazi na kuwa Mhasibu Mkuu wa UVCCM, kisha akateuliwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo (Tanzania Bara), na baadaye Kaimu Katibu Mkuu mwaka 2005. Alipochaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Novemba 3, 2007, siku ileile akateuliwa kuwa Mweka Hazina Mkuu wa CCM.

Kama alivyofanya uamuzi mgumu mwaka 2003 kwa kuacha ajira na mshahara mzuri katika Kiwanda cha Matofali cha Kisarawe, hatua ya kujitosa kugombea Ujumbe wa NEC mwaka 2007 – tena kupitia kundi gumu la Tanzania Bara – ulikuwa ni uamuzi mwingine mzito.

Katika chaguzi zote za NEC ya CCM tangu ianzishwe Februari 5, 1977, kundi hilo ndilo lililokuwa gumu kuliko yote kutokana na kuwa na wagombea wenye majina mazito nchini, nyadhifa kubwa katika chama na serikali yake na wafanyabiashara wakubwa.

Siku zote kunakuwa na viongozi wa juu kama Katibu Mkuu wa CCM, Naibu Katibu Mkuu, Wajumbe wa Sekretarieti ya Taifa, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri, naibu mawaziri (waliopo madarakani na wastaafu), wakuu wa mikoa na vigogo wengine lukuki nchini.

Wakati wagombea kutoka kundi hili huwa ni 60, lakini wanaopaswa kuchaguliwa kulingana na nafasi linazotengewa ni 20 na ndiyo maana mchuano wake huwa ni mgumu kupindukia.

Akiwa mmoja kati ya vijana wasiozidi watano mwaka 2007, Makalla aliwania nafasi hizo 20 za Ujumbe wa NEC akipambana na wenzake 59 na kushinda.

Alishinda akiwa bado mtoto akiwa na baadhi ya vigogo wa miaka mingi katika siasa za nchi hii wakiwa wameingia katika uongozi wa juu ukiwamo wa kitaifa kama akina Kanali Abdulrahman Kinana, Kapteni Jaka Mwambi, Kapteni John Chiligati, Kapteni John Komba, Luteni Edward Lowassa, Luteni Yussuf Makamba, Frederick Sumaye, William Lukuvi na kadhalika.

Aliwashinda pia wengi wakiwamo vigogo maarufu nje na ndani ya CCM, wengine wakiwa viongozi waandamizi wa chama hicho au mawaziri waliokuwa madarakani au wa zamani kama Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Profesa Juma Kapuya, Profesa David Mwakyusa, Dk. Mathayo David Mathayo, Dk. Diodorus Kamala, Emamnuel Mwambulukutu, Wilson Masilingi na wengineo.

Kama kiongozi wa kisiasa mahali popote, Makalla amekuwa akijipambanua siku zote kama mchapakazi hodari, msikivu na mwenye mahusiano ya karibu na maofisa na watumishi wote wa chini yake, huku akiwaheshimu kwa nidhamu ya hali ya juu wakuu wake wa kazi.

Ndiyo maana alipokuwa Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM kati ya mwaka 2005 na 2007, aliweka rekodi iliyokuwa haijawahi kufanywa na makatibu wakuu wote waliomtangulia.

Alipandisha na kuboresha kwa kiwango kikubwa mishahara na marupurupu mengine kwa watumishi wa kada zote, akaanzisha utaratibu wa posho za kila wiki kwa watumishi katika Makao Makuu ya UVCCM, akaanzisha utaratibu wa watumishi kupata chai kamili asubuhi ili kuongeza hamasa ya kazi kwao na alifanya mabadiliko mbalimbali makubwa ya msingi.

Katika kufanya hivyo, mengi yaliyokuwa hayatarajiwi wala kufikiriwa na yeyote yalifanyika, lakini kwa sababu ya utashi na msukumo wa fikra zake mwenyewe alibuni, kuthubutu na kufanya.

Alipochaguliwa kuwa Mjumbe wa NEC na kisha Mweka Hazina Mkuu wa CCM, Makalla alifanya kazi kubwa ya kukijenga kiuchumi chama hicho akishirikiana na viongozi wenzake.

Moja ya makubwa ni kuongeza mfumo wa vyanzo vya mapato. Pia alikuwa akiboresha na kusimamia mishahara na posho mbalimbali kwa watumishi na maofisa wa kada zote.

Namwangalia pia alivyo na ushirikiano mkubwa na watumishi wote katika ngazi zote. Halafu jambo kubwa jingine ni kuelekeza – tena bila kinyongo na wala kuchoka. Katika miaka yote niliyofanya naye kazi sikuwahi kumuona amenuna kwa namna zote hata pale panapostahili akasirike.

Aidha, upenzi wake mkubwa wa michezo takribani yote hususan soka na muziki, vinatoa nuru mpya na njema katika sekta hiyo kutokana na kuteuliwa kwake kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Amekuwa karibu na wanasoka wengi, makocha na timu zao kuanzia Simba ambayo ni mmoja kati ya mashabiki wake wa damu, na pia ni mpenzi mkubwa wa muziki kutoka wa dansi hadi wa kizazi kipya. Hii inamfanya mara kadhaa awe anafikia hadi kujitolea fedha zake mwenyewe kuzichangia sekta hizo zote.

Ndiyo maana ukienda katika Jimbo lake la Mvomero utashangaa kuwa ingawa lipo vijijini, lakini linakua kwa kasi kimichezo tangu achaguliwe kuliwakilisha bungeni mwaka 2010.

Ni rafiki wa karibu pia wa wamiliki, wahariri na waandishi wa habari na vyombo vyao. Hivyo uteuzi wake ni dhahiri utaiboresha sekta hii muhimu kwa maendeleo duniani kote.

Lakini licha ya hayo yote, Makalla katika upande wa pili ni mbaya kwa wazembe, wale wanaoharibu kazi na hasa kwa makusudi na kila anayependa kudhulumu watu. Hapokei kabisa majungu, fitina, uongo, usengenyaji na hataki kabisa ubaguzi.

Ukitaka kujua ubaya wake hata kama ataendelea kukuchekea, jaribu kufanya lolote kati ya hayo halafu uone. Huyo ndiye Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo aliteuliwa hivi karibuni.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0713 676 000 na 0762 633 244