Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati (EWURA) kwa huduma nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya.
Aidha Mhandisi Mramba amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kuisaidia Ewura ili iweze kutekeleza majukumu yake katika Mazingira wezeshi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba alipotembelea katika Banda la EWURA katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
“Tunachoweza kusema Ewura imefanya kazi nzuri sana mpaka sasa hivi, kama mnavyoona Huduma zinazodhibitiwa na Ewura zinapatikana na wameweza kudhibiti Upatikanaji wa Huduma yenyewe, bei inayotolewa na ubora wa Huduma hiyo.
“Kwenye eneo la bei nafikiri mnafahamu kuwa nchi yetu ni miongoni mwa nchi zenye bei ya chini sana ya Huduma za Umeme. Lakini Kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia kuwa Huduma za bei ya umeme zimezidi kuimarika, kule kukatika kwa umeme mara Kwa mara kumepungua,” amesema na kuongeza kuwa:
“Sisi kama Wizara ya nishati wajibu wetu kuhakikisha kwamba EWURA anafanya kazi yake kulingana na Sheria pamoja na Sera zilizowekwa,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dk. James Mwainyekule, amesema mwezi uliopita walisaini mkataba na Tanesco kupima utendaji kazi na namna ya utekelezaji kazi.
“Uwekezaji huu unafanywa na serikali ambapo hadi Juni 30, mwaka huu ubora wa mafuta ulifikia asilimia 97. Tunazingati bei katika soko la dunia tukifuatilia na kila mwezi bei zilishuka na kupanda kulingana na soko la dunia.
“Magari takribani 5,000 yanatumia gesi hadi sasa na hii imesaidia kwa asilimia kubwa kupunguza dola kutumika katika kiagiza mafuta nje, kwa sababu gesi hii ya mafuta inatoka nchini.”