Kwa masikitiko makubwa, nimepokea taarifa ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila ya Februari 13, 2013 kuwa Bunge linakusudia kuzuia urushaji wa matangazo ya moja kwa moja (live) ya redio na televisheni kutoka bungeni. Dk. Kashilila amesema ni kosa pia kuwapiga picha wabunge wakiwa wamesinzia bungeni.

Kwa maelezo yake, anawasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupata njia (channel) ya televisheni ya kurushia matangazo ya Bunge, yatakayorushwa baada ya kuhaririwa. Anadai baadhi ya wabunge wanazomoka na kufanya vituko kwa kujua kuwa wanarushwa moja kwa moja hewani.


Sitanii, kama ipo bahati mbaya katika dunia hii, basi ni pamoja na tangazo hili. Hatujasahau Tanzania imetokea katika mfumo wa chama kimoja kilichoshika hatamu hadi mwaka 1992. Mfumo huu ulijiegemeza katika ‘zidumu fikra sahihi za mwenyekiti wa….’


Uliifanya Serikali, Bunge na Mahakama kuendeshwa kwa usiri wa ajabu. Imethibitika mara zote kuwa usiri huzaa matumizi mabaya ya madaraka, ni kinyume cha misingi ya utawala bora na unatoa mamlaka yasiyostahiki kwa kikundi cha watu wachache wenye masilahi binafsi ya kufisadi nchi.


Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na imetia saini Tamko la Haki za Binadamu la Desemba 10, 1948 ambapo Kifungu cha 19 (Article 19) cha Tamko hili, kinatoa uhuru wa mtu kutoa na kupokea mawazo bila kujali mipaka ya nchi.


Sitanii, mabadiliko ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1984 ndiyo yaliyoliingiza katika Katiba Tamko hili la Haki za Binadamu. Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inaakisi Kifungu cha 19 cha Tamko la Haki za Binadamu kinachoruhusu uhuru wa mawasiliano na haki ya kupewa taarifa.


Mwaka 2010 Tanzania imetia saini Mpango wa Sherikali ya Uwazi (Open Government Partnership/Initiative) unaoongozwa na Rais Barrack Obama wa Marekani, na tayari Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba ipo kwenye mchakato wa kutunga Sheria ya Haki ya Kupata Habari, itakayoruhusu nyaraka zote za Serikali kuwekwa wazi kwa wananchi.


Kwa kusema kweli, stanii, kwa zaidi ya miaka 10 sasa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoka katika mazongwe na kadhia ya kuficha habari kwa kiwango cha kugonga mihuri ya siri hata barua za mialiko. Watanzania tumewafahamu vyema wabunge wetu kupitia utaratibu huu wa matangazo ya moja kwa moja.


Leo kwa masikitiko, Dk. Kashilila anataka kuturejesha enzi za ukoloni. Anawatetea wabunge wanaolala bungeni wasipigwe picha.


Ni wazi kuna upungufu katika Kanuni za Bunge zinazotokana na Sheria ya Haki, Kinga, Wajibu na Mamlaka ya Bunge ya Mwaka 1988. Kanuni hizi zirekebishwe na kuwabana wabunge wanaoharibu ustaarabu na utamaduni wa taifa hili.


Sikubaliani na mpango wa Bunge kwa asilimia 100 kuwaadhibu wananchi wasione kinachoendelea bungeni. Sikubaliani pia na nia ya kuhariri mijadala ya wabunge. Ikumbukwe kama si ufinyu wa nafasi na mfumo wa uwakilishi bungeni tunaoutumia, ilibidi wananchi sote tuingie bungeni na kutoa mawazo yetu.


Kwa maana nyingine wabunge ni wawakilishi wetu na hatuwezi kuruhusu kuwepo siri juu ya nini anazungumza au awepo mtu wa kuhariri alichozungumza mtu tuliyemtuma sisi (mbunge) na tunamlipa sisi kupitia kodi zetu.


Sitanii, suala la wabunge kulala bungeni na wakapigwa picha, nasema magazeti na televisheni zinazofanya hivyo zinastahili kupongezwa badala ya kulaumiwa. Bungeni si mahala pa kusinzia, ni mahala pa kuchapa kazi. Wabunge wanaotaka kulala usingizi wabaki hotelini na si kulala kwenye ukumbi wa bunge.

 

Nchi jirani ya Kenya wamefikia hatua vikao vya Baraza la Mawaziri, Bunge na kesi mahakamani vinarushwa hewani moja kwa moja. Hakuna siri katika kutumia kodi za wananchi. Leo tunataka kuzuia haki ya watu kupata habari? Haiwezekani.

 

Mwisho nasema nia ya kudhibiti (censorship), kuhariri na au kuzuia baadhi ya habari kutoka bungeni, kamwe haikubaliki popote. Wananchi simameni sawa na mlivyopinga suala la fao la kujitoa. Wanaanza kidogo kidogo hawa. Tukiwakubalia watapanga kuuza nchi bila sisi kufahamu maana watakuwa wamejifungia. KWA PAMOJA TUSEME USIRI BUNGENI HAPANA.