MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango amewaagiza wakuu wa wilaya za mkoa Kigoma kufuata maadili ya uongozi katika kutumia magari waliyokabidhiwa kwa kuleta tija katika kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi badala ya kutumika magari hayo kwenda baa.

DK Mpango ameema hayo Ikulu ndogo mjini Kigoma wakati akikabidhi magari kwa wakuu wa wilaya akiwa kwenye ziara ya kiserikali ya siku saba mkoani humo na kusema kuwa ni lazima magari hayo yatoe matokeo yanayopimika katika utendaji wa matumizi ya magari hayo.

Amesema amegundua bado wakuu wengi wa wilaya hawajui shida, kero na changamoto zilizopo kwa wananchi hivyo ni lazima magari hayo yatumike kufika kwa wananchi kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi.

“Tunataka magari yafanye kazi kusikiliza kero ili ziweze kumfikia Mama Samia na kufanyiwa kazi lakini nasema kuwa ni marufuku gari hizi kutumika kwenda baa ni lazima mzingatie miiko ya uongozi ili kuhakikisha zinafanya matumizi yaliyokusudiwa na zitunzwe,”amesema Makamu wa Rais.

Soma Hapa:http://Makamu wa Rais aagiza barabara kukamilika kwa wakati Kigoma

Awali Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Raisi Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Zaidi Katimba amesema serikali kupitia wizara hiyo imetoa magari hayo kwa wakuu wa wilaya ili kuondoa changamoto ya kuazima magari kwenye halmashauri na taasisi za serikali.

Amezitaja wilaya zilizokabidhiwa magari hayo kuwa ni pamoja na Kigoma, Uvinza, Kasulu, Kibondo na Kakonko.

Naibu Waziri huyo amesema magari hayo yatarahisisha utendaji wa viongozi hao katika kusimamia majukumu ya serikali na kufika kwa wananchi kwa urahisi.

Akizungumza katika wilaya Uvinza Dkt. Mpango ameuelekeza uongozi wa Serikali mkoani hapa kuwachukulia hatua watumishi watakaobainika kushiriki kuruhusu uingizaji wa mifugo wilayani Uvinza kinyume cha Sheria na kusababisha ongezeko la migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Amesema baadhi ya watumishi wa Umma wasio waadilifu wamekuwa wakipokea fedha kinyume na sharia ili kuwaruhusu wafugaji kuingiza mifugo wilayani humo bila kufuata taratibu zilizowekwa na serikali.

‘‘Mamlaka za vijiji zinapaswa kuzingatia Sheria na Kanuni za matumizi bora ya Ardhi pia nakuagiza Mkuu wa Mkoa pamoja na watendaji wako kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaohusika na zoezi hilo bola kuzingatia maelekezo ya serikali kuhusu taratibu za ufugaji kwani nchi haitegemei mifugo pekee’’ amesema Dkt. Mpango.

Sambamba na hayo kupitia ziara yake makamu wa Rais amekagua ujenzi wa barabara ya Malagarasi, Ilunde hadi Uvinza yenye urefu wa Km. 51.1ambayo ujenzi wake umefikia Asilimia 54 huku ikitarajiwa kukamilika Machi, 2025.

Mara baada ya kukagua mradi huo, Makamu wa Rais amemshauri Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha anatumia kipindi hiki cha kiangazi kukamilisha maeneo muhimu ya ujenzi wa barabara hiyo bila kuathiri ubora wa kazi.

Please follow and like us:
Pin Share