Na Isri Mohamed
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza na kusomewa shtaka moja la kulawiti, leo Jumanne Julai 09, 2024.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Erick Marley, Dkt Nawanda amesomewa shtaka hilo na waendesha mashtaka wa Serikali, Magreth Mwaseba na Martha Mtiti.
Kwa mujibu wa Mwaseba, Nawanda alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 154 (1)(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16.
“Mshtakiwa, Yahaya Nawanda, Mkazi wa Nyamata wilayani Bariadi mkoani Simiyu unashtakiwa kwa kosa la kumwingilia kinyume na maumbile ‘kumlawiti’ Tumsime Ngemela, kosa ulilolitenda Juni 2, 2024 eneo la maegesho ya magari lililoko Rock City Mall wilayani llemela mkoani Mwanza,” amesema Mwaseba.
Dkt. Nawanda ameachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana ya shtaka lake mpaka litakapotajwa tena Julai 16, 2024.