Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekubali maombi ya zuio la muda kwa Bodi ya Wadhamini ya CUF inayomuunga mkono Mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, katika shauri dogo namba 51/2017, lililowasilishwa mahakamani hapo na Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe.
Jaji wa Mahakama Kuu, Jaji Wilfred Ndyansobera ameipiga mafuruku bodi hiyo kufanya shughuli zozote zinazohusu chama cha CUF hadi shauri la msingi namba 13/2017 litakapomalizika.
Jaji Ndyansobera amedai kuwa, ametoa uamuzi huo mdogo baada ya kupitia hoja za mawakili wa pande zote mbili, na kujiridha kwamba maombi ya muombaji yalikuwa na nguvu kisheria, pamojw na kukidhi masharti yaliyowekwa kwenye kesi,
Awali Jaji Ndyansobera aliyatupilia mbali maombi ya Mawakili upande wa walalamikaji wakiongozwa na Wakili Msomi anayemuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Msomi, Gabriel Malata, ya kumtaka jaji asisome maamuzi hayo kwa madai kuwa wanakusudia kukata rufaa katika mahakama ya Rufaa juu ya maamuzi ya Jaji Ndyansobera kukataa kujitoa katika kusikiliza mashauri ya CUF, ambapo alisema hakuna hakuna hoja za kisheria zinazozuia mahakama kuacha kuendelea na shughuli zilizopangwa.