Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

IMEELEZWA kuwa hadi sasa taasisi nunuzi 1,147 zimeshajiandikisha kwenye mfumo mpya wa ununuzi wa kielektroniki (NeST) pamoja na wazabuni zaidi ya 22,000 kutoka katika makundi makuu matatu ambayo sheria mpya ya Mamlaka hiyo inataka yapate zabuni za serikali.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Tafiti, Maendeleo na Ubunifu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma nchini (PPRA), Mhandisi Masunya Nashon wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF).

Amesema, idadi hiyo ya taasisi na wazabuni wazawa waliojiandikisha kwenye mfumo inaonesha mwitikio mzuri katika matumizi ya mfumo huo mpya.

“Kwa hiyo ukiangalia kwa muda mchache tofauti na mfumo uliokuwepo kwa muda wa mwaka mmoja, tunaona idadi ya wazabuni waliojiandikisha ni wengi, na tunategemea kupata wazabuni wengi zaidi maana kadri tunavyopata wazabuni wengi kwenye maombi, ndivyo ushindani unavyokuwa mpana na uwazi,” amesema.

Hata hivyo amebainisha kuwa, katika maonesho ya Sabasaba mwaka huu wamekuja kuonesha watanzania shughuli za PPRA ikiwemo matumizi ya sheria mpya ya ununuzi, sheria namba 10 ya mwaka 2023, kanuni zake pamoja na matumizi ya mfumo wa ununuzi wa Umma NeST.

Mhandisi Nashon ametaja manufaa ya sheria mpya kuwa ni pamoja na kuongeza wigo wa maendeleo kwa wazawa ambao umegawanyika katika makundi Makuu matatu ,upendeleo kwa makundi maalum yaan vijana ,wanawake,wazee na watu wenye mahitaji maalum.

“Sheria mpya inaelekeza kila taasisi nunuzi serikalini kutenga asilimia 30 ya bajeti ya kuwezesha makundi hayo kushiriki katika makundi ya Serikali,” amesema.

Amefafanua kuwa, Serikali imeongeza wigo ambapo kwa sasa zile zabuni zote za shilingi bilioni 50 kushuka chini ni lazima ziende kwa wazawa .

Kwa mujibu wa Mhandisi Nashon, sheria hiyo pia inatoa upendeleo kwa ununuzi wa bidhaa za ndani kwa maana ya bidhaa zinazodhalishwa ndani ikiwa ni malighafi au chochote kinachozalishwa ndani.

“Hivyo Serikali imekuwa ikijenga uwezo kwa taasisi nunuzi juu ya sheria mpya, kanuni na mfumo wa ununuzi wa kielektroniki NeST. Sasa hivi mafunzo yamefanyika katika Mikoa ya Mbeya Morogoro, Iringa na Mwanza ni kwa ajili ya Taasisi nunuzi na wafanyabiashara,” amesema.

Vilevile amesema Serikali kupitia PPRA imekuwa ikiendelea kutoa mafunzo kwa makundi maalum ambapo Kwa mwaka jana walikuwa na kampeni ya kuelezea fursa ambazo zipo katika ununuzi wa Umma na walipata makundi mengi ambayo yalijiandikisha na yalikuwa na vigezo vilivyokidhi kwenye taasisi nunuzi.

“Yalipoletwa kwetu tuliyathibitisha na kuweka kwenye kanzidata ya Mamlaka na mpaka Juni 30 tulikuwa na makundi 427 kutoka katika yale makundi Makuu matatu,” amesema.

Ameongeza kuwa mfumo huo umeshaanza kutumika tangu Oktoba 2023 ambapo amesema wazabuni wanaweza kujiandikisha kupitia simu Janja mahali popote.

Ameziasa taasisi nunuzi watangaze fursa hizo kwenye mfumo wa NeST wazabuni waingie kwenye mfumo ili waweze kuona hizo fursa na mchakato utaendelea kwenye mfumo na mwisho wa siku apatikane mzabuni .

Please follow and like us:
Pin Share