Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Enock Tarimo amechora picha ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayomwelezea akiwa katika majukumu matatu ya kitaifa ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watembeleaji wa maonesho hayo ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.
Akizungumza katika maonesho hayo, amesema picha hiyo inamzunguzia Dk. Samia Suluhu Hassan katika majukumu yake makuu matatu ya kitaifa.
“Jukumu la kwanza la kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaiona picha ambayo ina ushungi mwekundu na vazi jeusi, analo jukumu la pili ambalo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi tunamuona katika vazi la chama, ana ushungi mweusi na vazi la kijani. Jukumu la tatu tunamuona Dk. Samia Suluhu Hassan Amiri Jeshi Mkuu yuko katika vazi la kijeshi,” amesema Tarimo.
Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Deograsia Ndunguru, amesema wanafunzi wanafundishwa mbinu mbalimbali za uchoraji na ufanyaji sanaa.
“Tumekuja na picha walizobuni wanafunzi na mapambo ambayo ni bunifu za wanafunzi, tunawafundisha uchanganyaji wa rangi, matumizi ya rangi zenyewe, kutumia fursa zinazowazunguka ili kujipatia kipato. Mfano kuna chupa za vinywaji mbalimbali ambazo tukishakunywa tunatupa, hizo takataka ni fursa kwa wanafunzi wetu, wanaokota na kutengeneza bidhaa mpya inayoweza kuwapatia kipato,” amesema Dk. Ndunguru.
Mmoja wa wahitimu katika fani hiyo, Sultan Samwel, amesema kumekuwa na dhana potofu na hata baadhi ya wazazi kudhani kwamba sanaa ni uhuni hali inayosababisha kuwapo kwa mwamko mdogo.
“Watu wengi walikuwa hawajui kama ngazi ya chuo kikuu mwanafunzi anaweza kujifunza kuchora, tunawatengeneza wanafunzi wakimaliza masomo waweze kujiajiri. Ajira zipo lakini hazitoshi, wanaomaliza ni wengi na si wote wanaweza kuajiriwa na serikali kwahiyo tunamuandaa mwanafunzi anapotoka anakuwa tayari ana kitu cha kufanya,” amesema.