Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
PROGRAMU ya Shule Bora nchini, imetoa msaada wa vifaa vya kujifunzia, vilivyogharimu sh. mil 40 kwa wanafunzi wa shule zilizoathirika na mafuriko Wilayani Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.
Pia imetoa msaada wa majiko banifu nane yenye thamani ya sh.milioni 29 kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali za utunzaji wa mazingira katika shule nne za msingi wilayani Mkuranga.
Akizungumza katika makabidhiano ya misaada hiyo, Ofisa elimu Mkoa wa Pwani, Sarah Mlaki alitaja msaada uliotolewa ni madaftari 38,000, kalamu za wino na kalamu za risasi ,utakaowafikia jumla ya wanafunzi 7,300 .
“Programu ya shule bora imetupatia msaada huu kwa ajili ya shule zetu zilizoathirika na mafuriko ni matumaini msaada huu utawasaidia wanafunzi wetu ,maana lengo la programu hii ni kuongeza ufaulu na kuimarisha elimu nchini”alielezea Mlaki.
Vilevile alifafanua ,msaada wa majiko katika wilaya ya Mkuranga itasaidia kupunguza athari za uchafunzi wa mazingira na kwamba bado mahitaji ya majiko hayo ni makubwa katika shule za mkoa wa Pwani.
Mratibu wa Programu ya shule Bora ofisi ya Rais TAMISEMI, Winfrid Chiluba, aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri hizo kuhakikisha msaada huo unawafikia walengwa Kwa haraka ili malengo yaweze kufikiwa.
Awali Mwakilishi wa Ubalozi wa Uingereza Getrude Mapunda
,alibainisha msaada huo kutolewa chini ya ufadhili wa nchi hiyo, wamelenga mwakani kuongeza fedha zaidi katika sekta ya elimu kwa serikali ya Tanzania ili kuimarisha utoaji wa elimu bora.
Nae Kaimu Katibu Twawala mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala, alishukuru programu hiyo kwa kuithamini Jamii ya Mkoa wa Pwani husuni kwa waathirika na kuzingatia utunzaji wa Mazingira.
Twamala alieleza, kupitia majiko hayo mkoa huo utaendelea kujijenga kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kupunguza madhara yatokanayo na kuni na mkaa kwenye Taasisi na Jamii kwa ujumla.
Kupitia misaada hiyo Kaimu Katibu Tawala huyo aliagiza Wakurugenzi kuhakikisha misaada hiyo inawafikia walengwa kwa wakati .
Mratibu wa programu ya shule Bora kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Winfrid Chilumba alielekeza ,vifaa hivyo vilivyotolewa kupelekwa kwenye maeneo ambayo yana mahitaji makubwa .
Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa Tisa nchini, inayotekeleza mradi wa Shule Bora ambao unatekelezwa kwa msaada wa Serikali ya watu wa Uingereza “UKaid” wakishirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) .
Mikoa inayotekeleza mradi huo ni Pwani, Tanga,Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi, Simiyu, Mara na Rukwa ambapo ulianza kutekelezwa April 2022.