Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
KAMISHNA wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Shukrani Kyando ametoa wito kwa wananchi kujitahidi kulipia gharama za upimaji ardhi ili waweze kupimiwa Viwanja vyao na kupewa Hatimiliki.
Wito huo ameutoa jana Julai 7, 2024 katika banda lao lililopo katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.
“Kwahiyo tunawashauri wananchi ambao wanamiliki Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na sehemu yoyote ile nchini wajitahidi sana kulipia gharama za upimaji kupitia makampuni ya urasimishaji au taasisi binafsi au ofisi za wakurugenzi, ili wapimiwe ardhi zao na baada ya hapo wapewe hatimiliki zao.
“Ni muhimu kupata hatimiliki kwaajili ya ulinzi wa ardhi zao. Kwasababu sasa hivi migogoro ni mingi usipokuwa na ulinzi wa kisheria kwenye ardhi yako unaweza ukajikuta umeipoteza…kwahiyo tunawashauri wananchi wafuate hizo taratibu,” amesema.
Hata hivyo amewashauri wanaouziana ardhi kuhakikisha fedha za malipo zinawekwa katika akaunti ili kuepuka utapeli.
“Haiwezekani kuuza ardhi ya Sh. milioni 200 kwa milioni 50, lazima ujiulize ni kwanini auze kwa bei hiyo? usinunue ardhi kwa kuwa inauzwa kwa bei ya chini unatakiwa kujiridhisha kwanza na fedha zote ambazo unanunua ardhi zipitie kwenye akaunti ya wauzaji ili ziweze kutengeneza ushahidi wa hayo mauziano.
“Kwa Mkoa wa Pwani tumebaini kwamba mauzo mengi wananchi wanapeana fedha mkononi, kwa hiyo wananchi wanatapeliwa na inakuwa ngumu kuthibitisha kwa sababu watu wengi wanakimbia na muda mwingine wanawageuka kwamba haukunipa fedha,” amesema na kuongezwa:
“Lakini kama zingepitia kwenye akaunti kunakuwa na ushahidi hata vyombo vya kisheria vinaweza vikachukua hatua kwasababu ushahidi unakuwepo na unakuwa wa wazi,”